BARAZA LA WAFANYAKAZI TSC LAPITIA UTEKELEZAJI WA BAJETI NA MAJUKUMU YA TUME
Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) limekutana kujadili na kupitia utekelezaji wa bajeti na majukumu ya Tume kwa mwaka wa fedha 2025/2026, pamoja na utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, Julai hadi Septemba 2026.
Mkutano huo Na. 1/2026/2027 umefanyika tarehe 5 Novemba 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, ukilenga kupitia mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na kuweka mikakati ya kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Tume.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Mwl. Paulina Nkwama aliwataka wajumbe kushiriki kikamilifu katika majadiliano na kutoa maoni yenye kujenga kwa niaba ya watumishi wanaowawakilisha.
Mwl. Nkwama alifafanua kuwa Baraza ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano kati ya Menejimenti na wafanyakazi, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji na mazingira ya kazi.
Katika neno la utangulizi, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Nuhu Mlekwa, alieleza kuwa mikutano ya Baraza inatoa fursa kwa wajumbe kupitia utekelezaji wa bajeti na mipango ya Taasisi, kujadili masuala ya ustawi wa wafanyakazi na kutoa mapendekezo yanayolenga kuboresha utendaji wa Tume.
Pamoja na mambo mengine, wajumbe wa mkutano huo walipitia taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Baada ya kupokea taarifa hizo, wajumbe walijadili na kutoa mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha mipango na utekelezaji wa majukumu ya Tume, kuimarisha matumizi bora ya rasilimali za umma na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa walimu na wadau wengine wa sekta ya elimu.
Aidha, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Tume wa kuimarisha afya na ustawi wa watumishi na kukabiliana na magonjwa sugu yasiyoambukiza, washiriki walipatiwa elimu kuhusu lishe bora na Afisa Lishe kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Bi. Jane P. Ndanga. Elimu hiyo ililenga kuwajengea watumishi uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia lishe bora katika kulinda afya zao.
Mkutano huo umehitimishwa kwa kusisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji, nidhamu na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya Tume. Wajumbe pia wamehimizwa kuhakikisha maoni na mapendekezo yanayotolewa katika Baraza yanazingatiwa na kufanyiwa kazi ili kuleta maboresho katika utendaji wa Taasisi na utoaji wa huduma bora kwa walimu nchini.