Kuajiriwa upya kwenye kazi ya Ualimu
KUAJIRIWA UPYA KWENYE KAZI YA UALIMU
Mwalimu aliyefukuzwa kazi na kutumikia adhabu kwa muda usiopungua miezi kumi na miwili, au aliyeacha kazi kwa utaratibu anaweza kuajiriwa upya chini ya kifungu cha 12(1) cha Sheria Tume ya Utumishi wa Walimu, 2015 na kifungu cha 17 (1) na (7) cha Sheria ya Tume ya Utumishi wa Umma, 2002.
Vigezo vinavyotakiwa ili Mwalimu aweze kuajiriwa upya.
Kwa kuzingatia Mwongozo / Maelekezo yaliyotolewa na kupitia barua ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yenye Kumb.Na.CCB/271/449/01/61 ya tarehe 05.01.2015 imetoa maelekezo ya namna ya kushughulikia maombi hayo. Mwalimu anayeomba kuajiriwa upya lazima awe amekidhi vigezo vifuatavyo:-
- Kutumikia adhabu kwa muda usiopungua miezi 12 (mwaka mmoja);
- Kuwepo na uthibitisho wa mwajiri mwenye nafasi wazi;
- Kuwa na wadhamini watatu;
- Maombi ya Mwalimu yawe yamejadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya Wilaya ya Kuajiriwa Upya na kuwepo kwa Muhtasari wa kikao husika hicho.
Utaratibu wa kushughulikia maombi ya Walimu wanaoajiriwa upya
- Mwalimu ataomba nafasi ya ajira kwa Mwajiri yeyote mwenye nafasi;
- Mwalimu atawasilisha maombi yake kwa Katibu wa Tume ngazi ya Wilaya ya kuajiriwa upya yakiambatishwa na barua ya Mwajiri mwenye nafasi pamoja na maelezo ya wadhamini wasiopungua watatu. Wadhamini hao wanaweza kuwa viongozi wa dini au Viongozi wa Serikali;
- Kamati ya TSC Wilaya itajadili maombi hayo na vielelezo vilivyowasilishwa na kuwasilisha Tume mapendekezo ya Walimu waliokidhi vigezo;
- Mapendekezo yatajadiliwa kwenye Mkutano wa Tume na maoni kuwasilishwa ili kupata kibali cha ajira kutoka kwa Katibu Mkuu Ofisi Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora OR-MUUUB;
- OR-MUUUB watawasilisha maombi kwa mwenye Mamlaka ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi na itamjulisha Mwalimu kuwa amekubaliwa au amekataliwa na nakala kutumwa kwa Katibu wa Tume.
- Mwalimu atawasilisha kibali kwa Mwajiri na kwa Tume ngazi ya Wialaya ili mchakato wa Ajira ufanyike.
Mambo muhimu ya kuzingatiwa: -
- Kanuni ya 48 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Walimu za mwaka 2016 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 89 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, ni wajibu wa Tume, mwajiri na Mwalimu kutunza vyema kumbukumbu zinazohusu ajira.
- Walimu wanaoajiriwa upya katika Utumishi wa Umma watakiwe kujaza upya mkataba wa ajira ingawa wataendelea kutumia namba zao za usajili za awali (TSC Namba). Mikataba hiyo iandikwe “re-engagement”.
- Mwalimu atakiwe kujaza nakala nne za mkataba ambapo nakala moja inabaki Wilayani, Nakala moja ibaki kwa mwajiri wake, Nakala moja anapewa Mwalimu na Nakala moja huletwa TSC Makao Makuu.
- Walimu wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza /walioruhusiwa kuajiriwa upya wakiwa na umri zaidi ya miaka 45 ajira zao ni za mkataba (Kanuni 19 ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003 / Kanuni za kudumu katika Utumishi wa Umma, 2009).
VIAMBATISHO
Kiambatisho Na.A1: Mkataba wa ajira ya masharti ya kudumu
Kiambatisho Na. A2: Fomati ya barua ya ajira ya masharti ya kudumu
Kiambatisho Na. B: Fomati ya Rejesta ya usajili wa Walimu kwa alfabeti
Kiambatisho Na. C1: Barua ya kuthibitishwa kazini
Kiambatisho Na. C2: Barua ya Msamaha wa kuthibitishwa kazini
Kiambatisho Na. D: Fomati ya rejesta ya kuthibitisha kazini Walimu
Kiambatisho Na. E: Barua ya kupanda cheo
Kiambatisho Na. F: Barua ya kujulishwa kutopandishwa cheo
Kiambatisho Na. G: Barua ya kubadilishwa cheo
Kiambatisho Na.H: Fomati ya rejesta ya kupandisha vyeo Walimu
Kiambatisho Na. I: Fomati ya rejesta ya Walimu waliobadilishiwa vyeo/kazi
Kiambatisho Na. J: Fomati ya rejesta ya Walimu walio masomoni.
Kiambatisho Na. K: Fomati ya TANGE
Kiambatisho Na. L1 na L2: Fomati ya rejesta ya Walimu waliohitimisha utumishi.
Kiambatisho Na. M: Fomati ya rejista ya masuala ya Pensheni, Mikataba na Mirathi.
Kiambatisho Na. N: Fomati ya rejesta ya Walimu walioajiriwa upya