MAKAMU MWENYEKITI WA TUME YA UTUMISHI WA WALIMU AFUNGUA AWAMU YA TANO YA MAFUNZO KWA WATUMISHI WA TSC

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Bi. Bahati Mgongolwa amefungua awamu ya tano ya mafunzo kwa Watumishi wa Tume yaliyowahusisha Maafisa na Watumishi wa Kada Saidizi yanayofanyika tarehe 26 – 29 Mei, 2025 katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Kampasi ya Tabora.
Katika ufunguzi huo, Bi Mgongolwa amewaagiza Watumishi wa Tume kuendelea kutoa elimu kwa walimu ili waweze kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Bi. Bahati alisema kuwa walimu wakizingatia maadili watasaidia kuandaa wanafunzi bora ambao watakuwa na tija katika maendeleo ya Taifa.
“Ni mara chache kukuta familia ya mwalimu ikiwa katika maadili mabaya lakini mara nyingi familia za walimu zinakuwa na maadili mazuri na sisi kama Tume tunaka walimu waendelee kuwalea watoto katika maadili mema,” alisema.
Katika hatua nyingine Makamu Mwenyekiti Bi. Bahati aliipongeza Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Walimu kwa kuendesha mafunzo kwa Watumishi wa Kada Saidizi kwa kuwa watumishi hao ni muhimu kwa maendeleo ya Taasisi yoyote.
“Mimi nawaona Kada Saidi kama viungo katika chakula …mmefanya jambo muhimu kuendesha mafunzo kwa watumishi hawa kwani itasaidia kuwajengea uwezo na kuboresha utendaji wao wa kazi kwa manufaa ya Tume katika kuwahudumia walimu,” alisema.
Aliwataka baada ya mafunzo hayo kufanya kazi kwa bidii ili kuifanya Tume kuwa kimbilio la walimu kutokana na huduma bora inayotolewa.
Makamu Mwenyekiti huyo aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma hususan katika suala la kutunza siri katika maeneo wanayofanyia kazi ili kuendelea kulinda hadhi na heshima ya Serikali.
“Nyie Madereva mnapokuwa na viongozi kwenye magari wakati mwingine wanapigiwa simu ya kikazi ni vema maneno mnayosikia yasitoke nje…sio unapotoka unakwenda kuwaeleza watu mazungumzo ya kiongozi wako. Hali kadhalika, Watumishi mnaohusika na utunzaji wa kumbukumbu za ofisi (masijala) na Waandishi Waendesha Ofisi mna nafasi kubwa ya kufahamu mambo mengi ambayo ni siri, jengeni tabia ya kuheshimu maadili ya kazi yenu,” alisema.
Awali Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina Nkwama alisema kuwa mafunzo hayo yanakamilisha kundi la mwisho la Watumshi ambao walikuwa hawajapata mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya misingi ya uadilifu katika utumishi wa umma, misingi ya utoaji wa huduma bora kwa watumishi na wadau na utaratibu wa utunzaji wa kumbukumbu na uendeshaji wa ofisi.
Alisema kuwa mafunzo hayo pia yatawajengea uwezo watumishi hao kuhusu usaidizi kwenye vikao na uandikaji wa taarifa, ushirikiano na mawasiliano kazini, nafasi ya kada saidizi katika mchakato mzima wa uendeshaji wa mashauri ya nidhamu na rufaa za walimu.
Aidha, Katibu wa TSC alisema kuwa baada ya Mafunzo kwa watumishi hao mafunzo yanayofuata ni kwa Wajumbe wa Kamati ngazi za Wilaya ambao hawajapata mafunzo hayo kwa kuwa lengo la Tume ni kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa kuwajengea uwezo watumishi wake.
Mwl.Paulina alisema kuwa mafunzo hayo yanawashirikisha Maafisa wa Tume kutoka Makao Makuu, Wilaya za Mkoa wa Dodoma, Iringa, Katavi, Kilimanjaro, Manyara, Rukwa, Shinyanga na Singida pamoja na Watumishi wa Kada Saidizi kutoka Ofisi za Tume nchi nzima.