BARAZA LA WAFANYAKAZI TSC LAPITIA UTEKELEZAJI NA MAKADIRIO YA BAJETI YA MWAKA 2026/2027

24 Mar, 2026
BARAZA LA WAFANYAKAZI TSC LAPITIA UTEKELEZAJI NA MAKADIRIO YA BAJETI YA MWAKA 2026/2027

Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) limekutana kujadili na kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi wa Tume hiyo.

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi aliwataka wajumbe kushiriki kikamilifu katika mijadala ya masuala ya bajeti ili kuhakikisha mipango ya Tume inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa watumishi katika kufanikisha majukumu ya Tume ya kusimamia masuala ya utumishi wa walimu nchini.

Katika neno la utangulizi, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi, Bw. Nuhu Mlekwa, alieleza kuwa kikao hicho ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa taratibu za usimamizi wa rasilimali za umma, ambapo wajumbe hupata fursa ya kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka unaoendelea na kutoa maoni kuhusu makadirio ya bajeti ya mwaka ujao.

Aidha, wajumbe wa kikao hicho walipata wasilisho kutoka kwa Afisa Uchumi wa Tume, Bi. Zaitun Ramadhani, ambaye aliwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Tume kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Katika wasilisho lake alieleza mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa bajeti hiyo.

Kwa upande mwingine, Afisa Uchumi Mkuu wa Tume, Bw. Elia Malaki, aliwasilisha mada kuhusu makadirio ya bajeti ya Tume kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akibainisha maeneo ya kipaumbele yatakayowezesha Tume kuendelea kuboresha huduma zake kwa walimu na wadau wengine wa sekta ya elimu.

Wajumbe wa Baraza walipata fursa ya kujadili mada zilizowasilishwa na kutoa mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha mipango ya Tume na kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi zaidi.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa wajumbe kusisitizwa umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya Tume ili kuendelea kutoa huduma bora kwa walimu na kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu nchini.