Kushughulikia Mafao na Mirathi ya hitimisho la kazi ya Ualimu
Mafao yanayolipwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
Watumishi wote wa Umma wakiwemo Walimu mafao yao ya kustaafu kazi kwa mujibu wa Sheria, kufariki au kuacha kazi kwa utaratibu wakiwa na miaka 15 katika utumishi yanalipwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF). Utaratibu wa kushughulikia mafao haya hufanywa na Mwajiri. Tume ya Utumishi wa Walimu itawasilisha kwa Mwajiri vielelezo na kumbukumbu muhimu za kiutumishi zitakazohitajika kwa ajili ya mchakato wa mafao hayo
Mafao ya hitimisho la kazi yanayolipwa na Hazina
Tume ina jukumu la kushughulikia Mafao ya Hitimisho la kazi kwa Walimu ambao hulipwa na Hazina. Mafao hayo ni kwa walimu waliostaafu/ kufariki kabla ya tarehe 01, Julai 2004, kipindi ambacho Sheria ya Hitimisho la Kazi ya mwaka 1999 haijaanza kutumika na mafao ya kiinua mgongo cha Walimu walioajiriwa kazi ya ualimu kwa masharti ya mkataba
Aina ya mafao hayo ni: -
-
Kiinua Mgongo kwa Walimu waliofanya kazi kwa Mkataba;
-
Pensheni kwa Walimu waliobadilisha kazi na kujiunga na Waajiri wengine kwa kufuata utaratibu wa kiutumishi kabla ya tarehe 01.07.2004
-
Mirathi ya Walimu waliofariki kabla ya tarehe 01.07.2004.
Mafao ya Kiinua mgongo cha Walimu walioajiriwa kwa Mkataba;
Kundi hili linajumuisha;
-
Walimu raia wa Tanzania waliomba na kupewa kibali cha kuajiriwa tena kwenye Utumishi wakiwa na zaidi ya miaka 45.
-
Wageni wa kazi (Wakimbizi). Hawa ni Walimu waliopata kibali cha kuishi na kufanya kazi Tanzania.
Utaratibu wa kushughulikia Ajira ya Mkataba
-
Mwalimu atawasilisha maombi yake ya ajira ya mkataba kwa Mwajiri akiwa ametimiza vigezo;
-
Mwajiri atahakikisha ana nafasi wazi ili aweze kuomba kibali cha ajira ya mkataba kwa Katibu Mkuu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora;
-
Mwajiri akishapata kibali UTUMISHI, Mwajiri na mwalimu wataingia Makubaliano kwa kujaza kikamilifu Mkataba wa Ajira ya Masharti ya Mkataba; Mkataba utakaojazwa ni ule ulio kwenye kifungu cha D.33 cha Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma, 2009;
-
Mkataba utawasilishwa kwa Katibu Mkuu UTUMISHI na Mwajiri;
-
Katibu Mkuu UTUMISHI atakamilisha Mkataba na kuurejesha kwa Mwajiri. Mwajiri atawasiliana na Katibu Msaidizi wa Wilaya na kuwasilisha nakala halisi ya Mkataba Tume Makao Makuu kwa ajili ya kuandaliwa barua ya ajira ya masharti ya mkataba
-
Mwalimu akihitimisha kipindi cha Mkataba, atawasilisha maombi ya mafao kwa Katibu wa Tume. Mchakato wa mafao ya kiinua mgongo yatashughulikiwa.
Vielelezo muhimu vinavyotakiwa kwa Walimu ili kuandaliwa mafao ya Mkataba.
- Mkataba halisi uliokamilishwa pamoja na viambatisho vyake ikiwemo kibali cha Katibu Mkuu - UTUMISHI;ii. Barua ya ajira ya mkataba;
- Picha 2 (Passport size);
-
Fomu za TISS;
-
Kivuli cha ATM Card;
-
Hati ya malipo ya mshahara (Salary Slip) ya mwezi wa kwanza wa kuanza mkataba na wa mwisho wa Mkataba;
-
Kiapo cha kuthibitisha Majina (kama yanatofautiana)
-
Uthibitisho wa kurejeshwa michango ya PSSSF kwa Mtumishi na Mwajiri (Kama alikuwa anachangia kinyume cha masharti ya ajira ya Mkataba);
-
Uthibitisho wa kulipa madeni mbalimbali (kama alikuwa anadaiwa).
Mafao ya Walimu wa Pensheni
Hawa ni Walimu waliofikia umri wa kustaafu wa miaka 60 ambao walibadilisha Kada na kujiunga na Waajiri wengine kwa kufuata taratibu za kiutumishi zikiwemo kuazimwa au kupewa likizo bila malipo kabla ya tarehe 01.07.2004.
Utaratibu wa kushughulikia mafao ya Walimu wa Pensheni
Mchakato wa kushughulikia mafao ya Walimu hawa huanzia kwa waajiri wao wa awali. Uzoefu unaonesha kuwa kwa sehemu kubwa Walimu hao walikuwa waajiriwa wa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Utamaduni kwa wakati huo. Ili kushughulikia mafao hayo:-.
-
Mwalimu lazima awe amestaafu kazi kwa lazima au kwa hiari katika Wizara/Taasisi ambayo alikuwa ameazimwa;
-
Mwalimu atamwandikia barua na Mwajiri wake wa awali kabla ya kuazimwa ili kuomba kulipwa mafao yake ya kipindi alichofanya kazi ya ualimu;
-
Mwajiri wa awali wa Mwalimu atawasilisha Tume ngazi ya Wilaya au Makao makuu maombi ya mafao ya Mwalimu husika;
-
Tume ngazi ya Wilaya au Makao makuu itafuatilia kumbukumbu zote za kiutumishi pamoja na vielelezo muhimu vinavyohitajika katika kushughulikia mafao ya Mwalimu. Aidha, itahitajika kupata Jalada la kituo (Station File) kutoka kituo cha mwisho alichokuwa akifanya kazi mtumishi. Msisitizo ni kwamba, Mwalimu anapopewa likizo bila malipo au ruhusa ya kuazimwa anapaswa kutimiza vigezo/masharti aliyopewa kwenye barua yake ya kuazimwa au kibali cha likizo bila malipo, ili kuondoa usumbufu wakati wa kuandaa mafao yake.
Vielelezo muhimu vinavyotakiwa kwa Walimu wa Pensheni
-
Barua ya Ajira ya masharti ya kudumu
-
Barua ya kuthibitishwa kazini kwa walimu walioajiriwa baada ya 1.1.1988 au barua ya kuthibishwa kazini kwa mujibu wa Sheria kwa walimu walioajiriwa kabla ya tarehe 1.1.1988.
-
Barua ya Cheo cha mwisho kabla ya kuazimwa/kuhamisha Utumishi wake
-
Barua / Kibali cha kuazimwa
-
Barua ya Ajira ya Taasisi / Mwajiri mpya
-
Uthibitisho wa kuchangiwa 25% kwa ajili ya kulinda Pensheni ya mwalimu kwa kipindi alichoazimwa.
-
Salary Slip ya mwezi wa mwisho kabla ya Kuhama/kuazimwa;
-
Kibali cha kustaafu kutoka Taasisi/Mwajiri alikohamia/azimwa;
-
Uthibitisho wa majina (kama yanatofautiana)
-
Fomu za TISS;
-
Kivuli cha ATM Card;
-
Picha 2 (Passport Size).
Mafao ya Mirathi ya walimu waliofariki kabla ya tarehe 01.07.2004.
Hawa ni Walimu waliofariki kabla ya tarehe 01.07.2004 ambao mafao yao hulipwa na Hazina. Mchakato wa kushughulikia mafao haya huanzia kwenye ngazi ya Wilaya.
Utaratibu wa kushughulikia mirathi
-
Mwajiri atawasilisha jalada la marehemu likiwa na taarifa za mirathi ya Mwalimu kwenye ofisi ya Tume ngazi ya Wilaya;
-
Tume ngazi ya Wilaya itafuatilia kwa Mwajiri vielelezo vyote vinavyotakiwa kisha kuwasilisha jalada hilo Tume Makao Makuu.
Vielelezo muhimu vinavyotakiwa ilikuandaa Mirathi.
-
Jalada la mtumishi husika la kituo (Station File);
-
Barua ya Ajira;
-
Barua ya kuthibitishwa kazini kwa walimu walioajiriwa baada ya 1.1.1988 au barua ya msamaha wa kuthibishwa kazini kwa mujibu wa Sheria, kwa walimu walioajiriwa kabla ya tarehe 1.1.1988;
-
Barua ya cheo cha mwisho kabla ya kufariki;
-
Kivuli cha cheti cha kifo kilichothibitishwa na Mahakama;
-
Hati ya Usimamizi wa Mirathi (Original) iliyobandikwa picha ya Msimamizi wa Mirathi na kugongwa muhuri wa Mahakama;
-
Muhtasari wa kikao cha ukoo cha kumteua Msimamizi wa Mirathi;
-
Nakala ya vyeti vya kuzaliwa watoto/viapo vya kuzaliwa watoto;
-
Uthibitisho wa ndoa ya marehemu (kiapo kutoka Mahakamani au nakala ya cheti cha ndoa);
-
Kiapo cha kutunza watoto chenye picha;
-
Kiapo cha kuthibitisha majina ya marehemu (kama yanatofautiana);
-
“Salary Slip” ya mwezi wowote ndani ya miezi mitano kabla ya kifo;
-
Fomu ya mgao wa Mirathi inayotolewa na Mahakama;
-
Fomu za TISS kwa warithi wote walio kwenye fomu ya mgao;
-
Nakala za kadi za benki (ATM) za warithi wote walio kwenye fomu ya mgao;
-
Picha 2 (Passport Size) za Msimamizi wa Mirathi, mtu anayetunza watoto na wategemezi wote.
Mchakato unaofanyika katika kushughulikia Mafao ya Pensheni, Mikataba na Mirathi kwa Walimu.
Katika kushughulikia masuala ya Pensheni, Mirathi na Ajira za Mkataba Tume Makao Makuu inatekeleza majukumu yafuatayo: -
Wajibu wa Makao Makuu
-
uhakikisha vielelezo vyote vinavyohusu Mikataba, Mirathi na Pensheni vinapatikana na kuwekwa kwenye jalada la Mwalimu husika;
-
Kufanya ukokotoaji wa Hesabu;
-
Kuandaa majalada yaliyokamilika na kuyapeleka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG);
-
Kuandaa majalada yaliyokamilika kutoka kwa CAG na kuwasilisha Hazina kwa ajili ya malipo;
-
Kujibu hoja mbalimbali kutoka kwa waajiri, CAG na Hazina.
-
Kushughulikia malalamiko mbalimbali ya Walimu yanayohusu masuala ya Pensheni, Mirathi na Ajira ya Mikataba.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ana jukumu la: -
-
Kukagua na kuthibitisha Hesabu zilizokokotolewa na Tume Makao Makuu;
-
Kubaini hoja na kuziandika kwenye majalada husika (kama zipo);
-
Kuwasilisha/kurejesha Majalada TSC Makao Makuu baada ya kukamilisha hatua zake.
Wizara ya Fedha Uchumi na Mipango (Hazina)
ina jukumu la: -
-
Kubaini hoja mbalimbali, kuzianisha kwenye majalada husika na kuziwasilisha Tume Makao makuu iwapo kuna hoja; na
-
Kulipa Mafao ya Walimu na kurejesha majalada Tume.