“MWALIMU NI CHIMBUKO LA KADA ZOTE NDANI NA NJE YA UTUMISHI WA UMMA,” – PROF. MURUKE AWATAKA WALIMU KUENDELEA KUIMARISHA ELIMU

Dodoma, – Akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Walimu Duniani tarehe 5 Oktoba 2025, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Prof. Masoud Hadi Muruke, aliwahimiza walimu nchini kujiheshimu, kuheshimiwa na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Prof. Muruke alitoa kauli hiyo katika Viwanja vya Kilimani jijini Dodoma wakati wa bonanza lililoandaliwa na Tume ya Utumishi wa Walimu na kuhuduriwa na walimu na wadau mbalimbali wa elimu ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani.
“Napenda kuwapongeza walimu wote kwa mchango wenu mkubwa katika malezi, elimu na maendeleo ya taifa. Mwalimu ni chimbuko la kada zote ndani na nje ya Utumishi wa Umma,” alisema Prof. Muruke, akisisitiza kwamba siku hiyo ni fursa ya kutambua hadhi ya walimu na mchango wao katika jamii.
Aidha, walimu walifurahia bonanza la michezo na mazoezi ya kukimbia (jogging) kutoka Bunge hadi Viwanja vya Kilimani, ikiwapa nafasi ya kubadilishana mawazo, kujenga mshikamano na kuimarisha afya zao.
Prof. Muruke aliwataka walimu kushiriki kikamilifu katika kujenga taifa, ikiwemo ushiriki katika uchaguzi mkuu, akisema walimu ni kioo cha jamii na wana nafasi ya kuhamasisha jamii kushiriki kwa amani na utulivu.
Alisisitiza kuwa maadhimisho hayo ni mwito wa kuenzi walimu, kuwawezesha na kuwatambua kama washiriki muhimu katika kuimarisha misingi ya demokrasia na maendeleo endelevu ya taifa.
“Tuwape walimu sauti na nafasi katika safari ya kujenga taifa imara lenye mshikamano wa kweli,” alimalizia Prof. Muruke.