TUME YA UTUMISHI WA WALIMU YAADHIMISHA SIKU YA MWALIMU DUNIANI KWA KISHINDO

13 Oct, 2025
TUME YA UTUMISHI WA WALIMU YAADHIMISHA SIKU YA MWALIMU DUNIANI KWA KISHINDO

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeadhimisha Siku ya Mwalimu Duniani kwa kishindo jijini Dodoma kwa kuandaa maonesho ya huduma, vipindi vya ueleimishaji kwenye vyombo vya habari na bonanza la michezo lililowashirikisha walimu, viongozi wa serikali na wadau wa mbalimbali wa elimu.

Maadhimisho hayo yayohitimishwa Oktoba 5, 2025 yaligawanyika katika sehemu mbili tatu — maonesho ya huduma mbalimbali katika Viwanja vya Nyerere Square kuanzia Oktoba 1 hadi 5, 2025, ziara za kutoa elimu kwenye vyombo vya habari na bonanza la michezo lililofanyika katika Viwanja vya Kilimani likihitimisha rasmi maadhimisho hayo kwa shamrashamra, burudani na michezo ya kirafiki.

Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu, akifuatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa TSC, Prof. Masoud Hadi Muruke, Katibu wa Tume, Mwl. Paulina Nkwama, Kamishna wa Tume, Bi. Mariam Mnilwa, na Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Dkt. Suleiman Ikomba.

Walimu na wadau mbalimbali wa elimu kutoka Mkoa wa Dodoma walihudhuria, wakionesha mshikamano na hamasa kubwa ya kusherehekea siku yao.

 

Siku ya Duniani

Siku ya Mwalimu Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Oktoba, ikiwa ni kumbukumbu ya kutiwa saini kwa Mapendekezo ya mwaka 1966 kuhusu Hali ya Walimu (ILO/UNESCO Recommendation concerning the Status of Teachers). Maadhimisho haya yalianzishwa rasmi mwaka 1994 na UNESCO kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa lengo la kuenzi mchango wa walimu katika maendeleo ya elimu na jamii.

Malengo makuu ya maadhimisho haya ni pamoja na kutambua mchango wa walimu katika malezi na elimu, kuibua mijadala kuhusu changamoto zao, kuhamasisha vijana kujiunga na ualimu, na kuwapa walimu jukwaa la kujadili mustakabali wa taaluma yao.

Kwa mwaka huu, maadhimisho nchini Tanzania yamebebwa na kaulimbiu isemayo: “Wezesha walimu kuchagua viongozi bora kwa elimu na mafunzo stahiki.” Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha walimu kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kuchagua viongozi watakaoweka kipaumbele katika sekta ya elimu.

Tume ya Utumishi wa Walimu – Mhimili wa Ustawi wa Walimu

Tume ya Utumishi wa Walimu ni chombo cha kisheria kilichoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu, Sura ya 448, chenye jukumu la kusimamia ajira, maadili na maendeleo ya walimu wa shule za msingi na sekondari Tanzania Bara.

Tume ina ofisi 139 katika ngazi ya wilaya, huku makao makuu yake yakiwa Mtaa wa Mtendeni, jijini Dodoma. Kazi zake kuu ni pamoja na kuthibitisha ajira za walimu, kuwabadilishia vyeo, kupandisha cheo, kusimamia nidhamu na kutoa vibali vya kustaafu au kujiendeleza kielimu.

Katika utekelezaji wa majukumu hayo, Tume hutumia miongozo na waraka wa Serikali, ikiwemo Waraka wa Maendeleo ya Utumishi Na. 1 wa mwaka 2014, unaoelekeza kanuni na vigezo vya ajira na kupandishwa vyeo. Aidha, Tume hutoa mafunzo elekezi kwa walimu wapya na waliopo kazini kuhusu maadili na maendeleo yao kiutumishi.  

 

Maonesho na Bonanza

Tume iliandaa maonesho ya huduma mbalimbali katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kuanzia Oktoba 1 hadi 5, 2025. Maonesho hayo yalihusisha wadau muhimu wa elimu na taasisi za kijamii, zikiwemo Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF), Benki ya CRDB, na Wakala wa Huduma ya Damu Salama.

Huduma zilizotolewa ni pamoja na ushauri wa kiutumishi, huduma za kifedha, elimu ya hifadhi ya jamii na uchangiaji damu kwa hiari, ikiwa ni sehemu ya kuchochea utu na ubinadamu katika jamii.

Shamrashamra za maadhimisho zilikamilishwa kwa Bonanza la michezo katika Viwanja vya Kilimani, lililojumuisha michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, kuvuta Kamba, mbio za magunia, kukimbiza kuku, nk Bonanza hilo lililenga kuimarisha afya, urafiki na umoja miongoni mwa walimu na wadau wa elimu.

Maadhimisho ya mwaka huu yamekuwa ni kielelezo cha namna walimu wanavyothaminiwa kama mhimili wa elimu na maendeleo ya taifa. Kupitia maonesho na bonanza la kitaifa, Tume ya Utumishi wa Walimu imeonesha dhamira ya dhati ya kuwatambua, kuwaenzi na kuwawezesha walimu kuboresha taaluma yao na maisha yao kwa ujumla.