WATUMISHI TSC WATAKIWA KUSAIDIA WALIMU KUEPUKA KUKOPA KUPITA KIASI

23 May, 2025
WATUMISHI TSC WATAKIWA KUSAIDIA WALIMU KUEPUKA KUKOPA KUPITA KIASI

Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wametakiwa kutoa elimu kwa walimu ili kujiepusha na vitendo vya kukopa kupita kiasi jambo ambalo linaadhiri utendaji wao wa kazi.

Agizo hilo limetolewa tarehe 22 Mei, 2025 mjini Tabora na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Dkt. Emmanuel Shindika wakati akifunga awamu ya nne ya mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa za Walimu kwa Watumishi wa Tume kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo.

Alisema kuna baadhi ya walimu wanaojiingiza katika mikopo isiyo rasmi bila kuzingatia taratibu zinazosimamia watumishi wa umma na hivyo kujikuta wakishindwa kujikimu kimaisha na kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kufundisha kama inavyohitajika.

“Saidieni kundi hili (walimu) kwa kuwapa elimu na ushauri wa namna na kiwango cha kukopa kinachoruhusiwa kwa mujibu wa Sheria Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma. Kuna baadhi ya walimu hawawezi kutulia shuleni na kufundisha kila wakati wanaishi kwa wasiwasi kutokana na kudaiwa. Unakuta mshahara ukiingia wote unaishia kwenye kulipa madeni”, alisema.

Aliongeza kuwa “Ongezeni usimamizi wa karibu, kuna changamoto nyingi walimu wanakumbana nazo katika jamii. Wapo walimu ambao wanarubuniwa na watu wasiokuwa waaminifu na hivyo kujikuta wanatapeliwa. Tuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha walimu wetu wanakuwa katika mazingira salama wakati wote.”

Akitoa salamu wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo, Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Dkt. Hadija Mcheka alimpongeza Katibu wa TSC kwa kuona umuhimu wa kuwajengea uwezo watumishi hao na kueleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi hususan katika kushughulikia mashauri ya nidhamu ya walimu. 

“Naipongeza Tume chini ya Katibu wake, Mwl. Paulina Nkwama kwa kufiria kuweka haya mafunzo ambayo ni muhimu kwa ajili ya kutatua changamoto ambazo tulikuwa tunaziona kwa watumishi wetu katika kushughulikia mashauri ya nidhamu ya walimu,” alisema.

Aliongeza kuwa “ni imani yangu kuwa kila mshiriki ameongeza ujuzi ambao utamsaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kutenda haki katika kuamua masuala ya walimu.”

Alisema kuwa maamuzi ya mashauri yanayofanywa bila kuzingatia taratibu yanasababisha kutotendeka kwa haki pamoja na kuisababishia hasara serikali pale rufaa inaporudishwa ili shauri lianzishwe upya.

Akitoa neno la kumkaribisha mgeni rasmi kufunga mafunzo hayo, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina Nkwama alisema kuwa Mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa watumishi wa Tume kubadilisha utendaji kazi wao uwe wa kuzingatia taratibu zote katika kuendesha mashauri ya nidhamu.

“Tumekaa hapa kwa siku nne kuanzia tarehe 19 – 22 Mei, 2025 na washiriki wamepitishwa katika mada mbalimbali. Madarasa yetu yalikuwa mazuri na washiriki walikuwa na ushirikiano mkubwa. Imani yetu ni kwamba kuanzia sasa hakuna rufaa zitakazorudishwa kuanza upya kutokana na kutozingatiwa kwa taratibu,” alisema.

Alisema kuwa mafunzo hayo yanaendelea kutolewa kwa watumishi ambao bado hawajafikiwa wakiwemo baadhi ya wajumbe za Kamati za Tume za Wilaya kwa kuwa lengo ni kuhakikisha kila mtumishi wa Tume anapata mafunzo hayo.

Nkwama alisema mafunzo hayo yanafanyika chini ya ufadhili wa wadau wa Maendeleo, SIDA kupitia mradi wa Uboreshaji Kada ya Ualimu (Global Partinership for Education Teachers’ Support Program (GPE TSP) chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi Na Teknolojia na Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Katika hatua nyingine, Mwl. Nkwama alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazofanya kuhakikisha Sekta ya Elimu inapiga hatua kimaendeleo ikiwa ni pamoja na jitihada zakr za kushughulikia na kutatua kero mbalimbali za walimu.

“Watumishi wakiwemo walimu 386,479 wamepandishwa vyeo na kubadilishiwa kada katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, miongoni mwao wapo ambao wamepandishwa cheo zaidi ya mara moja huku wengine wakipandiswa kwa mserereko. Hii ni hatua ambayo inapaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo,” alisema.

Mwl. Nkwama alieleza mafanikio mengine ya Rais Samia katika Sekta ya Elimu kuwa ni kuboreshwa kwa miundombinu ya shule, wanafunzi kuongezewa muda wa kuhudumiwa na bima ya afya kutoka miaka 18 hadi 21, ongezeko la idadi ya wanafunzi wanufaika wa mikopo vyuo vikuu, kukamilika na kuanza kutumika kwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na Mtaala mpya unaozingatia ujuzi kwa elimu msingi na sekondari.