MWENYEITI TSC AKEMEA WATUMISHI WANAOSAMBAZA TAARIFA ZA SERIKALI KINYUME NA TARATIBU

30 May, 2025
MWENYEITI TSC AKEMEA WATUMISHI WANAOSAMBAZA TAARIFA ZA SERIKALI KINYUME NA TARATIBU

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Masoud Hadi Muruke amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa umma wakiwemo walimu ya kusambaza taarifa za serikali kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Hivyo, amewaagiza watumishi wa TSC kutoa elimu kwa walimu juu ya umuhimu wa kutunza siri za ofisi pamoja na madhara yanayoweza kutokea kwa mtumishi kwa usambazaji wa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kinyume na taratibu.

Prof. Muruke ameyasema hayo tarehe 29 Mei, 2025 wakati akifunga awamu ya tano ya mafunzo kwa Watumishi wa Tume yaliyowahusisha Maafisa na Watumishi wa Kada Saidizi yaliyofanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 26 – 29 Mei, 2025 katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Kampasi ya Tabora.

“Siku hizi tunaona mambo mengi ya ofisi yanarushwa kwenye mitandao. Mimi nimesikia kuna barua za walimu zipo kwenye mitandao, nikajiuliza ni nani kapeleka? Lakini inawezekana ni wao wenyewe kwa sababu hawana uelewa wa kutosha kuwa moja ya mambo ya msingi katika maadili ya utumishi wa umma ni pamoja na kutunza siri za ofisi.”

“Hivyo, baada ya mafunzo haya mnapaswa kwenda kuwaelimisha walimu wetu kuhusu umuhimu wa kuwa wazalendo, kutotumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa za ofisi pamoja na madhara yanayoweza kumpata mwalimu kwa kukiuka taratibu za kutoa taarifa za Serikali,” alisema.

Moja ya mambo yaliyofundishwa katika mafunzo hayo ni menejimenti ya utambuzi wa hisia katika kusimamia uendeshaji wa mashauri ya nidhamu ambapo Prof. Muruke alisema mada hiyo ilitolewa ili kusaidia watumishi wa Tume kutumia ubinadamu katika kuwahudumia walimu.

“Wakati wa kufanya kazi zetu tuwe binadamu, tukukumbuke kwamba walimu wanaoletwa mbele yetu nao ni binadamu, ni wafanyakazi na wanapitia changamoto nyingi. Hivyo, tunapaswa kuwa sehemu ya kuwasaidia ili wawe watumishi wenye maadili badala ya kila wakati kufikiria kuwachukulia hatua za nidhamu wanapokosea,” alisema.

Aidha, kiongozi huyo alisema kuwa watumishi wa Tume wanapaswa kuwa na maadili ili wawe mfano wa kuigwa kwani wao ndio wanaosimamia nidhamu ya walimu huku akifafanua kuwa mtumishi asiyekuwa na nidhamu hawezi kusimamia nidhamu kwa wengine.

Awali, akitoa neno la kumkaribisha Mwenyekiti huyo, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina Nkwama alisema kuwa baada ya awamu ya tano ya mafunzo hayo kukamilika watumishi wote wa TSC ikijumuisha Maafisa na Watumishi wa Kada Saidizi wamepatiwa mafunzo.

Alisema kuwa wazo la kutoa mafunzo hayo kwa watumishi wote wa Tume lilitokana na kuwepo kwa changamoto ambazo ziliibua malalamiko kutoka kwa walimu hususan katika uendeshaji wa mashauri ya nidhamu.

Changamoto ya kwanza ilikuwa ni ucheleweshaji wa haki kutokana na ucheleweshaji wa ushughulikiaji wa mashauri ya nidhamu. Jambo lingine ilikuwa pale ambapo masuala ya mashauri yanachakwatwa lakini hayafiki mwisho kwa ufasaha kutokana na kutozingatiwa kwa sheria, kanuni na taratibu hivyo kusababisha kuelekezwa na Tume kuanzishwa upya,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Kwa hiyo hizi changamoto kuu mbili na uelewa ambao ulikuwa hafifu kwa watumishi wa Tume, ilionekana kuwa ni vyema watumishi wote wapate mafunzo kwa lengo la kuwawezesha kupata uelewa wa utekelezaji wa majukumu yao, lakini pia kupata miongozo ambayo wataitumia kama rejea katika majukumu yao ya kazi.”

Katibu huyo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa watumishi kujengewa uwezo na kutoa maelekezo kwa Tume kutekeleza jambo hilo ambapo alieleza kuwa kwa upande wa watumishi wa Tume agizo hilo limetekelewa kwa asilimia 100 kwa kuwa watumishi wote wamepatiwa mafunzo.