WAZIRI MCHENGERWA AKABIDHI MAGARI 10 TSC, 9 YAPELEKWA OFISI ZA WILAYA

13 Aug, 2024
WAZIRI MCHENGERWA AKABIDHI MAGARI 10 TSC, 9 YAPELEKWA OFISI ZA WILAYA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa amekabidhi magari 10 kwa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) huku magari tisa (9) yakipelekwa katika Ofisi za TSC ngazi ya Wilaya.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magari hayo iliyofanyika tarehe 11 Agosti, 2024 katika Ofisi za TAMISEMI Mtumba jijini Dodoma, Waziri Mchengerwa alisema kuwa Serikali inatambua kuwepo kwa  uhitaji mkubwa wa magari katika Ofisi za TSC 139 zilizopo katika kila wilaya nchini.

Alisema kuwa magari 10 yaliyotolewa ni mwanzo  wa kuanza kuboresha mazingira ya utendaji kwa Makatibu Wasaidizi ili waweze kutekeleza mjukumu yao kwa ufanisi.

Ikumbukwe kuwa Serikali imekwisha toa magari kwa Makatibu Tawala Wasaidizi Seksheni ya Elimu wote nchini, Wakuu wa Divisheni za Elimu Msingi na Sekondari wote na sasa tumeanza kwa Makatibu Wasaidizi wa TSC wa Wilaya,” alisema.

Alisema lengo  la kutoa magari hayo ni kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za elimu zinazofanyika katika ngazi ya shule pamoja na kuwafikia walimu katika vituo vyao ili kuwasilikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.

Mhe. Mchengerwa alisema kuwa jukumu la usimamizi wa Elimu linahitaji uwajibikaji na usimamizi thabiti katika ngazi ya Taifa, Mikoa, Halmashauri, Kata na Shule.

Alisema kuwa pamoja na bidii, weledi, ubunifu, uaminifu na utiifu, mafanikio katika usimamizi wa elimu yanategemea pia uwezeshwaji wa vifaa na vitendea kazi ikiwemo vyombo vya usafiri.

Mhe. Mchengerwa aliongeza kuwa matarajio ya Serikali ni kuwa, magari waliyokabidhiwa yatakuwa nyenzo muhimu kwa viongozi wakiwemo Makatibu Wasaidizi  wa Wilaya katika usimamizi na ufuatiliaji wa Elimu nchini ikiwa ni pamoja na utatuzi wa kero zinazojitokeza.

Aidha , Waziri alielekeza kuwa magari hayo yatunzwe vizuri ili kuweza kuongeza ufanisi na ubora wa elimu katika utekelezaji wa majukumu ya kuwahudumia walimu ili wapite salama katika mzunguko wao wa ajira.

Mhe. Mchengerwa alisema kuwa baada ya kupata magari hayo hakutakuwa na visingizio vya kushindwa kutembelea walimu katika kusikiliza na kutatua changamoto zao badala ya kuwasubiri wawafuate ofisini.

Aidha, Mhe. Mchengerwa alisema kuwa kwa ofisi za Tume ambazo hazijapata magari, zinatakiwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kuwafikia walimu kwa kutumia vitendeakazi vilivyopo pamoja na kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmasahauri katika maeneo yao ili walimu waendelee kupata huduma bora.

“Nimeshaelekeza na leo ninarudia tena kuelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri kwa watumishi wa TSC waliopo katika maeneo yao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Pale wanapohitaji kuwafikiwa walimu, wakurugenzi wawapatie magari ili kazi za TSC zisikwame. Katibu Mkuu hakikisha hotuba yangu inawafikiwa wakurugenzi wote nchini ili agizo hilo litekelezwe kikamilifu,” alisema Waziri Mchengerwa.

Mhe. Mchengerwa aliwaagiza viongozi walikabidhiwa magari   kuhakikisha yanatumika kwa kuzingatia miongozo ya Serikali na yakayatunza ili yadumu.

Magari hayo yamenunuliwa chini ya Mradi wa BOOST ambapo Ofisi za Wilaya zilizopata Magari hayo ni Ilala, Tanga, Mbeya, Nyamagana, Rufiji, Kaliua, Bukombe, Kilosa na Ruangwa huku gari moja (1) ikitumika Ofisi za TSC Makao Makuu.