BUNGE LAPITISHA TRILIONI 9.1 BAJETI YA OFISI YA RAIS TAMISEMI KWA MWAKA 2023/2024

20 Apr, 2023
BUNGE LAPITISHA TRILIONI 9.1 BAJETI YA OFISI YA RAIS TAMISEMI KWA MWAKA 2023/2024

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Tume ya Utumishi wa Waalimu (TSC), Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 yenye jumla ya shilingi trilioni 9.1

Akitoa maelezo kuhusu hoja za wabunge zilizojitokeza wakati wa kujadili hotuba ya Bajeti ya Ofisi hiyo bungeni jijini Dodoma tarehe 18 Aprili, 2023,  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Angellah Jasmine Kairuki amesema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi 2022/23 Serikali iliidhinisha  kiasi cha shilingi bilioni 280.35 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya vyumba vya madarasa 8,252, maabara 2,745, mabwalo 86, mabweni 433, vituo vya afya 52 na zahanati 1,419 ambavyo utekelezaji wake kwa kiasi kikubwa umekamilika. 

Waziri Kairuki   alifafanua kuwa  katika mwaka wa fedha wa 2023/24 Serikali imetenga  jumla ya Shilingi bilioni 20.56 kwa ajili ukamilishaji wa maboma ya zahanati 376, mabweni 10 na bwalo 1  ambapo Serikali inaendelea  kufanya tathimini ya mahitaji halisi ya maboma ambayo hayajakamilishwa na  yale yanayoendelea kujengwa ili kuyawekea mpango wa kuyakamilisha kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumzia Sekta ya Afya, Waziri Kairuki alisema katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24 Serikali imetenga Shilingi Bilioni 116.92 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba lakini pia Serikali itaendelea kununua vifaa, vifaa tiba, dawa na vitendanishi kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Aidha, amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari zitahakikisha maeneo yenye changamoto ya mtandao yanafikiwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kuboresha mifumo iliyopo kama mfumo wa MUSE kwa usimamizi na matumizi ya fedha za Umma, TAUSI kwa ukusanyaji na usimamizi wa mapato, PlanRep kwa Mipango na Bajeti na utoaji wa taarifa za Halmashauri na mifumo mingine.