DKT. MSONDE AELEKEZA MaDED WOTE NCHINI KULIPA MARA MOJA MADAI YOTE YA WALIMU.

25 Apr, 2023
DKT. MSONDE AELEKEZA MaDED WOTE NCHINI KULIPA MARA MOJA MADAI YOTE YA WALIMU.

Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Majiji na Manispaa wameelekezwa kulipa mara moja madai yote ya Walimu ambao mpaka sasa hawajalipwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uhamisho kwani zoezi hilo pia lilifanyika ili kuboresha na kuimarisha utendaji kazi kwa dhima ya kuendelea kupaisha matokeo chanya ya Sekta ya Elimu nchini.

 

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Charles Msonde, alipokua akifungua Kikao Kazi cha Wadau kutoa maoni kuhusu kupitia Sheria na Kanuni zote zinazosimamia Utumishi wa Walimu kinachofanyika Mkoani Morogoro kwa siku nne kuanzia Aprili 24, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Ualimu Morogoro (Kigurunyembe).

 

“Ninatoa wito kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Majiji na Manispaa kulipa mara moja madai yote ya Walimu ambao mpaka sasa bado hawajalipwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uhamisho. Hatutaki Walimu wetu wawe na madai yoyote yale kwani mazoezi yote yaliyofanyika na kuleta madai hayo yalifanyika kwa dhamira njema ya Serikali katika kuendelea kuboresha na kuimarisha utendaji kazi kwa dhima ya kuendelea kupaisha matokeo chanya ya Sekta ya Elimu nchini.” Alisema Dkt. Msonde

 

Aliongeza kuwa wale wote wanaohusika na mnyororo mzima wa ulipaji wa madeni hayo watekeleze na kutimiza wajibu wao kama inavyotakiwa ili kuondoa malalamiko na ya kulimbikiza madeni ya Walimu yasiyo na tija kwa Serikali na kuunga mkono juhudi kubwa za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuiimarisha sekta hii ya elimu.

 

Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo akirejea mmomonyoko wa hivi sasa wa maadili nchini, alisisitiza Utatu katika malezi na maendeleo ya elimu kwa wanafunzi nchini akiwahusisha Wazazi, Walimu na Jamii kuwa ni muhimu sana katika kuwapatia weledi na maadili watoto wa Taifa la Tanzania kwa maendeleo chanya endelevu.

 

Dkt.Msonde alisema kuwa popote palipo na mazingira na elimu bora daima huleta matokeo chanya na bora na hivyo ni lazima elimu bora ipatikane kupitia kwa Walimu wa Taifa hili wenye mazingira bora na ili hilo liendelee kufanikiwa basi Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwa eneo lake la majukumu iliyokasimiwa bado ina kazi kubwa ya kufanya katika kufikia matokeo haya.

 

Akiainisha sehemu ya mafanikio ambayo Serikali imeyapata kupitia TSC katika kipindi cha miaka miwili alisema, “Jumla ya Walimu 160,868 walipandishwa vyeo, Walimu 24,888 waliajiriwa na siku chache zilizopita hivi karibuni kibali cha ajira za Walimu 13,130 kimetolewa na Mhe. Rais ikiwa ni jitihada zake na dhamira yake ya dhati kuendelea kuimarisha elimu nchini.”

 

Vilevile Dkt. Msonde alisema kutokana na kupitishwa na kuanza kutumika kwa Sera ya Elimu bila Malipo; mwaka 2021/2022 idadi ya wanafunzi iliongezeka mara mbili ya ile ya awali iliyotarajiwa na hivyo kusababisha Shule za Sekondari kutotosheleza idadi hiyo ya wanafunzi na Serikali kutenga zaidi ya Shilingi Bilioni 300 zilizojenga shule kote nchini na kutosheleza mahitaji.

 

“Katika jitihada hizo Serikali kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha uliopita ilitenga jumla ya Shilingi Bilioni 160 kujenga madarasa mengine zaidi baada ya kuonekana kuongezeka kwa wanafunzi zaidi wanaotakiwa kujiunga na masomo jambo lililoashiria mwamko zaidi wa jamii katika kupata elimu kutokana na kuimarika kwa mazingira na Sekta nzima ya elimu nchini.” Alisema Naibu Katibu Mkuu

 

Akielezea miradi inayoendelea kupitia Wadau wa Maendeleo katika Sekta ya Elimu nchini, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka OR-TAMISEMI, Dkt. Msonde alisema Mradi wa SEQUIP umetenga jumla ya Shilingi Trilioni 1.2 katika kuboresha sekta hiyo huku huku jumla ya Shule 1,026 zikijengwa kote nchini, Shule 232 za Kata zilizo karibu zaidi na wananchi zimejengwa, Shule 26 za Bweni kwa Wasichana zinajengwa huku jumla ya Shule 184 ikiwa ni shule moja katika kila Halmashauri zimeidhinishwa zijengwe huku Shule 10 kati ya hizo zikielekea kwenye ukamilifu.

 

Akizungumzia Mradi wa BOOST, Dkt. Msonde alisema jumla ya Shilingi Trilioni 1.15 zimetengwa kwa kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wake ambao umelenga kuboresha na kuimarisha Elimu Msingi na Awali ikiwa ni pamoja na kujenga Shule za Msingi 302, Madarasa 3,338 na Nyumba za Walimu 41.

 

Akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwenyekiti wa TSC, Prof. Willy Komba alisema wadau walioshirikishwa ni katika kikao kazi hicho ni sehemu ya uwakilishi kutoka Wizara, Taasisi za Serikali na Taasisi zisizokuwa za Serikali ambazo kwa namna moja au nyingine zinamgusa Mwalimu.

 

Prof.Komba alisema kuwa Tume ina imani kubwa sana kupitia uwakilishi huo itaweza kuwa na andiko ambalo litabeba maudhui ambayo yatatoa mwelekeo kwa Serikali wa namna bora ya kusimamia Utumishi wa Walimu.

 

Naye Katibu na Mtendaji Mkuu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama alitoa maelezo ya awali ya Kikao Kazi hicho alisema Tume imeandaa kikao hicho cha Wadau kwa siku nne kwa ajili ya kupata maoni na mtazamo kuhusu namna bora ya kusimamia Utumishi wa Walimu kwani wadau walioshirikishwa ni dhahiri kuwa ni watu mahiri wenye taaluma na uzoefu wa kutosha.

 

Tume ya Utumishi wa Walimu imeundwa kwa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448, na ilianza kutekeleza majukumu yake rasmi Julai 01, 2016 ikiwa ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari waliopo kwenye Utumishi wa Umma Tanzania Bara.