IDADI YA WATEJA WANAOTEMBELEA BANDA LA TSC YAZIDI KUONGEZEKA

04 Aug, 2022
IDADI YA WATEJA WANAOTEMBELEA BANDA LA TSC YAZIDI KUONGEZEKA

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeendelea kupokea idadi kubwa ya wateja wanaotembelea banda lake lililopo ndani Uwanja wa John Mwakangale katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa jijini Mbeya.

Idadi ya watu wanaotembelea banda hilo imeendelea kuongezeka kutokana na ubora wa huduma zinazotolewa na watumishi wa TSC waliopo kwenye banda la Tume hiyo inayosimamia Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari walio kwenye Utumishi wa Umma ambao idadi yao ni zaidi ya nusu ya watumishi wa Umma nchini.

Watumishi wanaotoa huduma kwenye banda hilo ni Mecktildis Kapinga ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu, Efraem Kamendu, Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Mbeya, Donatus Nungu, Afisa Sheria pamoja na Asha Lubuva ambaye ni Afisa anayeshughulikia Maadili na Nidhamu ya Walimu kutoka TSC Makao Makuu.

Baadhi ya wateja waliofika kwenye banda la TSC walieleza kuwa walitembelea banda hilo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wenzao ambao ni walimu walioridhishwa na elimu waliyoipata pamoja na kutatuliwa changamoto za kiutumishi zilizokuwa zinawakabili.

“Kuna wenzetu walikuja jana walikuwa na changamoto za kiutumishi, walitueleza kuwa walipokelewa vizuri, wakasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi wa changamoto zao. Lakini pia walituambia walipatiwa elimu ya mambo mbalimbali yanayohusu utumishi wa mwalimu ambayo hawakuwa na uelewa nayo. Hivyo, na sisi tukaona tufike wenyewe kwa kuwa tunahitaji huduma pamoja na kupata uelewa mpana juu ya utumishi wetu,” alisema mmoja wa wateja ambaye ni mwalimu.

Baada ya kupatiwa huduma, wateja hao walionesha kuridhishwa na namna changamoto zao zilivyofanyiwa kazi pamoja na kupatiwa elimu zaidi ya masuala ya kiutumishi huku wakiahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuwahabarisha wenzao ili wafike kwenye banda hilo kupata huduma za TSC.

“Tumehudumiwa vizuri na pia tumepatiwa elimu ya mambo mengi ambayo hatukuwa na uelewa nayo. Elimu tuliyoipata hapa itatusaidia kutekeleza majukumu yetu ya ualimu, hivyo tutazingatia sheria, kanuni na taratibu katika kufundisha wanafunzi,” alieleza mmoja wa wateja waliotembelea banda hilo.

Mbali na kutembelewa na walimu, banda la TSC limeendelea kuwa kivutio kwa wateja wa aina mbalimbali ambao wanafika kwa lengo la kupata uelewa juu ya kazi zinazofanywa na Tume hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2016.