KATIBU TSC ATOA WIKI MOJA KWA TSC WILAYA YA RUNGWE KUWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAKE

04 Aug, 2022
KATIBU TSC ATOA WIKI MOJA KWA TSC WILAYA YA RUNGWE KUWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAKE

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama ametembelea ofisi ya TSC Wilaya ya Rungwe iliyopo Mkoa wa Mbeya na kutoa muda wa wiki moja kwa watumishi wa ofisi hiyo kuwasilisha kwake taarifa ya utekeezaji wa majukumu ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Nkwama ametoa agizo hilo hivi karibuni wilayani hapo alipofanya ziara kwa lengo la kufanya ufuatiliaji wa namna wilaya hiyo inavyowahudumia walimu wa shule za Msingi na Sekondari za Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 na Kanuni zake za mwaka 2016.

Akiwa ofisini hapo, Nkwama alionesha kutoridhishwa na taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo iliyotolewa na mtumishi wa TSC Wilaya ya Rungwe, Paul Kazinde kutokana na kuwepo kwa mkanganyiko wa takwimu huku alieleza kuwa taarifa hiyo haikuzingatia mwongozo wa uwasilishaji wa taarifa uliotolewa na TSC Makao Makuu.

“Kwa kweli sijaridhishwa na namna taarifa yenu mlivyoiandaa, tulileta kwenu mwongozo wa namna ya kuandaa taarifa lakini hapa hamjazingatia. Hata takwimu mnazotoa hazipo sawa, zingatieni utaratibu uliotolewa kwani ni njia rahisi ya kuandaa taarifa inayokidhi mahitaji. Hivyo, ninawapa wiki moja muwasilishe kwangu taarifa iliyokamilika na iliyozingatia mwongozo unaotumika,” alisema Nkwama.

Kiongozi huyo aliendelea kueleza kuwa Ofisi za Wilaya zinatakiwa kuwa kimbilio la walimu na hivyo ni wajibu wa watumishi wa TSC ngazi ya Wilaya kuhakikisha wanachukua jukumu la kufuatilia masuala ya walimu kwenye mamlaka nyingine na hatimaye kutoa mrejesho kwa mwalimu husika ili kuondoa kero na usumbufu kwa mwalimu.

“Tunataka mwalimu anapowasilisha hoja yake sisi ndio tunajukumu la kwenda kugonga milango ya ofisi zingine kufuatilia hoja yake. Hatupaswi kuanza kumwambia mwalimu fuatilia mwenyewe. Siyo sawa kuona mwalimu anaacha jukumu lake la kufundisha wanafunzi anahangaika kwenye ofisi mbalimbali kufuatilia masuala yake mwenyewe wakati TSC tupo. Tunapaswa tubadilike na tuache tabia ya kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Katibu huyo.

Pamoja na hayo, Katibu huyo alionesha na kuridhishwa na namna Wilaya hiyo ilivyofanya kazi ya kutoa elimu kwa walimu kitu ambacho kimesababisha hali ya nidhamu kuimarika na kupungua kwa mashauri ya nidhamu huku akieleza kuwa jitihada zaidi zinahitajika ili walimu wawajibike zaidi katika kutoa huduma kwa wanafunzi.

“Ninawapongeza kwa namna mnavyotoa elimu kwa walimu, nimefurahi kusikia mmewafikia walimu wengi na kuwapa elimu juu ya masuala yanayohusu utumishi wao. Tunapaswa kuwahamasisha zaidi walimu ili waweze kuwajibika kikamilifu katika kufundisha wanafunzi. Wakati mwingine unaweza ukajisifu kuwa walimu wamepata elimu na wananidhamu nzuri lakini kama wanafunzi hawafaulu kazi yetu inakuwa haijakamika,” alisema Nkwama.

Kiongozi huyo pia alitembeleea Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ambapo alifanya mazungumzo na Mwanasheria wa Halmashauri hiyo ambaye alikuwa anamwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo.

Katika mazungumzo yao, Katibu wa TSC alieleza umuhimu wa Ofisi ya Mkurugenzi ambaye ndiye mwajiri wa mwalimu kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya TSC Wilaya kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha 14 (3) cha Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Na. 25 ya Mwaka 2015.