KATIBU TSC AWATAKA WASTAAFU KUENDELEA KUTOA USHAURI WA UBORESHAJI UTENDAJI WA TUME

19 Apr, 2024
KATIBU TSC AWATAKA WASTAAFU KUENDELEA KUTOA USHAURI WA UBORESHAJI UTENDAJI WA TUME

Katibu wa Tume ya utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama amesema Tume hiyo itaendelea kupokea na kutumia ushauri wa watumishi wastaafu wa TSC kwa ajili kuendelea kuboresha utendaji kazi wa Taasisi hiyo ili iendelee kutoa huduma bora kwa walimu.

Mwl. Paulina ametoa kauli hiyo leo tarehe 9 Aprili, 2024 wakati wa halfa fupi ya kuwapongeza na kuwapa mkono heri wastaafu 15 wa TSC ambao utumishi wao umekoma kwa mujibu wa Sheria hivi karibuni.

“Tunawathamini, tunawapenda wazee wetu kwa mchango mkubwa mliotoa wakati wa utumishi wenu ndani ya Tume…milango iko wazi, kwani tutaendelea kupokea ushauri wenu kwa ajili ya kuboresha zaidi utendaji wetu katika kuwahudumia walimu,” amesema.

Akitoa salamu kwa niaba ya Wastaafu wenzake, Bw. Michael Ndyamukama aliushukuru uongozi wa Tume ya Utumishi wa Walimu kwa kutambua mchango wao na kuamua kuwapa mkono wa kwa heri.

Amesema utamaduni huo ni mzuri kwani zipo Taasisi nyingi ambao hazina utaratibu wa kuwaita Wastaafu na kuwaaga baada ya utumishi wao kukoma.

Aidha, Bw. Ndyamukama ameupongeza uongozi wa TSC kwa mabadiliko makubwa ambayo yameboresha utendaji wa Watumishi wake.

Watumishi Wastaafu ambao wamepewa mkono wa kwa heri na TSC baada ya utumishi wao kukoma kwa mujibu wa Sheria ni Nusura Khamis Hiza, Michael Ndyamukama, Amiri Maulid, Faustina Kokuberwa na Mashaka Athuman.

Wengine ni Emiliana Mwabukusi, Joyce Paul Mwanga, Julius Joseph Nchimbi, Rose Pius Nyahinga, Patricia Binde, Juma Athuman Chite, Nelson Wambura, Boaza Cheyo, Daima Mwakwenda na Mwanaisha Said Idd.