MAAFISA WA TSC WATAKIWA KUWA WALEZI WA WALIMU

23 May, 2025
MAAFISA WA TSC WATAKIWA KUWA WALEZI WA WALIMU

Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) ngazi za Wilaya wametakiwa kuwa walezi wa walimu kwa kuwekeza nguvu katika kutoa wa elimu ili kuzuia walimu kutenda makosa ya kinidhamu yanayohatarisha utumishi wao.

Kauli hiyo imetolewa tarehe 19 Mei, 2025 mjini Tabora na Mweyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Prof. Masoud Hadi Muruke wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa mashauri ya nidhamu na rufaa za walimu kwa Maafisa wa Tume ngazi za Wilaya kutoka mikoa 9 nchini.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa ni muhimu kwa watumishi wa TSC kujenga ukaribu na walimu, kufahamu changamoto zao na kuwaelimisha kuhusu Sheria, Kanuni na Taratibu katika kushughulikia masuala ya kiutumishi.

“Ni muhimu sana kuelewa kwamba kipaumbele cha Tume ni kuhakikisha walimu hawafukuzwi kazi, hatupaswi kukaa kusubiri walimu wakosee ili tuwachukulie hatua za kinidhamu. Hivyo, ni lazima tuongeze nguvu katika kutoa elimu ili walimu wetu wasijikute wanakiuka maadili ya kazi yao, alisema kiongozi huyo.

Prof. Masoud alisisitiza kuwa Ofisi ya Tume ngazi ya Wilaya ikiwa na mashauri mengi ya nidhamu siyo kipimo kwamba inatekeleza majukumu yake vizuri kwa kuwa lengo ni kuhakikisha walimu hawatendi makosa hivyo, inapotokea walimu wanakiuka sana taratibu za kazi ni wazi kuwa Ofisi ya TSC haijatekeleza wajibu wake wa kuwa mlezi kwa walimu kama ilivyokusudiwa.

“Tumieni nguvu kubwa katika kuzuia makosa yasitokee kwa kuziba nyufa badala ya kusubiri kuja kujenga ukuta…msipende kujisifu kwa wingi wa mashauri ya kinidhamu katika maeneo yenu bali mjisifu kwa kuwa walimu wana uelewa wa kutosha juu ya taratibu za utumishi na hivyo hawatendi makosa,” alisema.

Aidha, Prof. Muruke aliwataka Maafisa wa Tume wanaohudhuria mafunzo kuzingatia masomo yote ambayo watafundishwa ili kuhakikisha wanatenda haki wakati wa kushughulikia mashauri ya kinidhamu dhidi ya walimu.

Akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina Nkwama aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya elimu nchini ikiwemo kuiwezesha Tume kuandaa Mwongozo wa Usimamizi wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa za Walimu na Mwongozo wa Mafunzo Elekezi Kwa Walimu Wapya.

“Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa katika maendeleo ya elimu nchini…sisi ni wanufaika na juhudi za Rais kwani katika kipindi chake amepandisha vyeo walimu wote waliokuwa na sifa za kupandishwa. Pia, madai mbalimbali ya walimu yakiwemo malimbikizo ya mishahara, fedha za uhamisho na fedha za likizo yameendelea kulipwa,” alisema.

Aliongeza kuwa hata mafunzo hayo ya siku nne ni matokeo ya juhudi za Serikali za kuwajengea uwezo Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Taifa ili waweze kuongeza ufanisi na weledi katika kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Mwl. Paulina alisema kuwa katika siku nne za mafunzo washiriki watafundishwa masuala muhimu katika utendaji wao wa kazi ambayo ni usimamizi wa nidhamu kwa walimu katika ngazi za shule, utaratibu wa kushughulikia mashauri ya nidhamu kwa walimu, utaratibu na hatua za kushughulikia masuala ya nidhamu yenye jinai, utaratibu na hataua za rufaa kwa ngazi TSC Makao Makuu na kwa Rais.

Alisema kuwa mada nyingine ni menejimenti na utambuzi wa hisia katika kusimamia uendeshaji wa mashauri ya nidhamu na fafanuzi kuhusu mwongozo wa mafunzo elekezi ya awali kwa walimu wapya.

Mafunzo hayo yanayoendeshwa chini ya ufadhili wa Programu ya kuboresha kada ya ualimu (Global Partnership for Education for Education Teachers’ Support Profram - GPE TSP) na kuendeshwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yamewahusisha Maafisa wa TSC Makao Makuu na wengine kutoka Ofisi za Wilaya za Mikoa ya Mwanza, Tabora, Kagera, Mara, Simiyu, Geita, Kigoma, Arusha na Njombe.