MENEJIMENTI ZA TAASISI ZA OR TAMIMSEMI ZATAKIWA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA PEPMIS KWA WATUMISHI WA CHINI

16 May, 2024
MENEJIMENTI ZA TAASISI ZA OR TAMIMSEMI ZATAKIWA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA PEPMIS KWA WATUMISHI WA CHINI

Menejimenti za Taasisi zilizoko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) zimetakiwa kuwawasaidia na kuwasimamia watumishi walio chini yao katika kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Utendaji wa Kazi wa Watumishi wa Umma -PEPMIS/PIPMIS kwa kuzingatia maelekezo ili kuleta ufanisi.

 Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Dkt. Wilson M. Charles tarehe 15 Mei, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku tatu yanayohusu ufuatiliaji wa Matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Utendaji wa Kazi wa Watumishi wa Umma (PEPMIS/PIPMIS) kwa Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo na Wakurugenzi Wasaidizi walioko katika Taasisi zilizoko chini ya OR – TAMISEMI.

 Alisema kuwa mfumo huo umejengwa katika misingi wa kuwasaidia watumishi  kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika shughuli za umma na vilevile kupata huduma mbalimbali ikiwemo kupata mikopo katika Taasisi za Fedha na kufuatilia uhamisho kwa urahisi bila urasimu.

 Dkt. Charles aliongeza kuwa matumizi ya Mfumo huo yamesaidia kudhibiti na kuondoa watu ambao waliokuwa wakiwatapeli baadhi ya watumishi kwa kuwaomba  fedha kwa kiwango cha kuanzia shilingi milioni moja na kuendelea kwa madai ya kuwa watawatafutia uhamisho huku wakighushi saini za Viongozi akiwemo Katibu Mkuu ofisi ya Rais TAMISEMI na Katibu Mkuu (UTUMISHI).

 Alisema hali hiyo imesababisha madhara mbalimbali ikiwemo usumbufu kwa watumishi ambao walikuwa wakitapeliwa kwa kuhamia katika Kituo ambacho walikwenda bila utaratibu huku mishahara yao ilibaki katika vituo vyao vya awali.

 Kwa upande wa Mkurugenzi wa Utawala wa Utumishi wa Umma - Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Felister Emmanuel Shuli aliwataka viongozi wa Menejimenti za Taasisi zote ambazo ziko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa watumishi wote ambao hawajasajiliwa katika Mfumo huo kutekeleza jukumu hilo ili kuepuka kuondolewa katika utumishi wa umma kwa kudhaniwa kuwa ni watumishi hewa.

 Aliongeza kuwa kuanza kwa Mfumo kumesaidia kuwabaini na kuwachukulia hatua baadhi ya Watumishi wasiozingatia maadili waliokuwa wakishirikiana na vishoka kuchukua fedha za watumishi kuanzia kiasi cha shilingi milioni moja hadi shilingi milioni tano kwa madai ya kuwatafutia uhamisho ili waende Taasisi ambazo wanadhani kwa maoni yao zina maslahi mazuri.

 Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Walimu ni miongoni mwa Taasisi ambazo zimeshiriki mafunzo hayo wakiongozwa na Katibu wa Tume, Mwl. Paulina Nkwama.