MHE. ZAINAB TSC ENDELENI KUSIMAMIA MAADILI YA WALIMU

03 Nov, 2024
MHE. ZAINAB TSC ENDELENI KUSIMAMIA MAADILI YA WALIMU

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Mhe. Zainab Katimba (Mb) ameitaka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuendeleza jukumu lake la msingi la usimamizi wa utumishi na Maadili ya Walimu.

 

Ametoa kauli hiyo tarehe 25 Septemba, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa niaba wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb) ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati za Wilaya za Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kutekeleza majukumu yao.

 

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwa na walimu wenye kujituma na wanaozingatia maadili ya kazi yao kwa ajili ya kuwalea Watoto kwa usahihi na hivyo kuboresha elimu nchini.

 

Mhe. Zainab aliwataka washiriki kutumia mafunzo yenye mada zinazohusu Muundo na Majukumu ya Tume, Majukumu ya Kamati za Wilaya pamoja na taratibu katika ushughulikiaji wa mashauri ya nidhamu na Rufaa kwa Walimu kuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kila siku ya Tume na Serikali kwa ujumla.

 

Alielekeza kuwa baada ya mafunzo hayo kila mhusika anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo na kuenda haki kwa walimu.

 

“Naomba nirudie kuipongeza Tume kwa kazi nzuri mnayoifanya... Naomba sote kwa pamoja tuendelee kutekeleza kauli mbiu ya “Kazi iendelee”. Kauli mbiu hii naomba itekelezwe kwa ufanisi na uadilifu na sisi kama Serikali tutaendelea kuwa pamoja nanyi katika kuhakikisha kwamba tunatoa ushirikiano wa kutosha,” alisisitiza.

 

Aidha, Mhe. Zainab alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuhakikisha kuwa, Wizara na Taasisi zinazosimamia Utumishi wa Walimu zinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzipatia fedha, nyenzo na watumishi wenye ujuzi na weledi wa kutosha ili kuboresha Sekta ya Elimu Nchini.

 

Awali, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Prof. Masoud Hadi Muruke alisemakuwa Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati za Wilaya yanafanyika katika Kanda mbalimbali ambapo Kanda ya Kaskazini itahusisha mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga huku Kanda ya Mashariki ikihusisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

 

Alisema kuwa kwa Kanda ya Kati mafunzo hayo yanahusisha Wilaya za mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora, Singida na Dodoma; Kanda ya Ziwa ina mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita; na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mafunzo hayo yanajumuisha wilaya za mikoa ya Rukwa, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa na Mbeya. 

 

Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Toba Nguvila alisema kuwa Walimu wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuhakikisha anatatua changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa zikiwakabili walimu ikiwemo za kuwapandishwa madaraja.

 

Aliwataka Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuhakikisha wafanyakazi kwa juhudi katika kumsaidia Rais kwenye usimamizi wa nidhamu, mashauri na madaraja kwa walimu kwa ajili ya maendeleo ya Nchi.