MWENYEKITI NA WAJUMBE WA TSC WAAPISHWA NA KUANZA KAZI RASMI

14 Jun, 2024
MWENYEKITI NA WAJUMBE WA TSC WAAPISHWA NA KUANZA KAZI RASMI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 13 Juni, 2024 amewaapisha viongozi mbalimbali aliowateuwa hivi karibuni katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

 

Miongoni mwa viongozi walioapishwa ni Prof. Maosud Hadi Muruke ambaye Rais Samia alimteua tarehe 15 Mei, 2024 kuwa mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) akichukua nafasi ya Prof. Willy Lazaro Komba ambaye muda wake ulimalizika.

 

Mara baada ya Rais Samia kumuapisha Mwenyekiti wa Tume, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Mohamed O. Mchengerwa (Mb) amewaapisha Makamishna nane (8) aliowateua hivi karibuni kuwa wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Walimu.

 

Waziri amefanya uapisho huo tarehe 13, Juni 2024 katika Ofisi za OR – TAMISEMI zilizopo jengo la Sokoine jijini Dodoma ambapo walioapishwa ni Bi. Mariam Gerald Mwanilwa kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Huruma Elias Mageni kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Bi. Hadija Mcheka kutoka OR – TAMISEMI na Bi. Mariam Rashid Haji kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 

Wajumbe wengine ni Bi. Bahati Shabani Mgongolwa kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Agrey Adelbert Mleli kutoka Baraza la Taifa la Ufundi na Mafunzo (NACTIVET), Bi. Jane Nikusomoka Mtindya kutoka Chama cha Walimu Tanzania na Bw. Lameck Philipo Mahewa kutoka Chama cha Walimu Tanzania.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mchengerwa alimtaka Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wa Tume hiyo kuhakikisha wanamaliza kero na changamoto za walimu ikiwemo ucheleweshwaji wa kupandishwa madaraja na walimu kucheleweshwa kubadilishiwa cheo baada ya kujiendeleza kielimu.

 

Waziri Mchengerwa alisema ana imani kuwa viongozi hao watafanya maboresho makubwa katika utumishi wa walimu ili walimu waendelee kufanya kazi kwa amani na utulivu huku akisisitiza kuwa nia ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona changamoto zote za walimu zinamalizwa na walimu wanatendewa haki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

 

“Tunakupongeza Prof. Muruke kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu, sisi tunakuamini. Walimu ni watu muhimu sana kwenye Taifa letu, na wewe umeletwa hapa makusudi ili kwa kushirikiana na Wajumbe na Sekretarieti ya Tume mfanye maboresho makubwa ili kumaliza changamoto za walimu. Sitarajii kusikia kwenye kijiji, kitongoji au shule yoyote kuna mwalimu ambaye changamoto zake hazijashughulikiwa,” alisema Waziri Mchengerwa.

 

Mara baada ya uapisho, Wajumbe hao wa Tume wameingia katika utekelezaji wa majukumu ya TSC kwa kuanza Mkutano wa Tume unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete ambapo masuala mbalimbali ya  yanayohusu utumishi wa walimu yataamuliwa.