NITAENDELEZA MIPANGO ILIYOANZISHWA NA WATANGULIZI WANGU: WAZIRI KAIRUKI

07 Oct, 2022
NITAENDELEZA MIPANGO ILIYOANZISHWA NA WATANGULIZI WANGU: WAZIRI KAIRUKI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb) amesema ataendeleza mipango yote iliyoanzishwa na Mawaziri waliomtangulia katika ofisi hiyo ili kuhakikisha Serikali inakamilisha mipango yake ya Maendeleo kwa kasi zaidi.

Waziri Kairuki amayasema hayo Oktoba 6, 2022 wakati akizungumza na Watumishi wa OR – TAMISEMI pamoja na Taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo katika hafla ya kumkaribisha Waziri huyo na kumuaga aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Innocent Bashungwa ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofayika katika ofisi za OR – TAMISEMI Mtumba, jijini Dodoma, Waziri Kairuki alisema kuwa Waziri Bashungwa na Mawaziri wengine waliomtangulia walifanya kazi nzuri na ndiyo maana miradi mingi ya Serikali imetekelezwa kwa ufanisi, hivyo anaamini kuwa mipango waliyoianzisha ni mizuri nayeye ataendelea kuiboresha ili kuleta mafanikio zaidi kwa wananchi .

“Ninatambua mawaziri waliotangulia wamefanya kazi kubwa katika Ofisi hii, na mimi ninawaahidi kuwa nitaendeleza mipango yote ambayo wenzangu waliianzisha kwa lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi. Mimi sio mtu ambaye nikiingia ofisi mpya napangua kila kitu walichoanzisha wenzangu, ni lazima tuwe na mwendelezo wa kile kilichoanzishwa ili tufikie malengo,” alisema.

Kairuki aliongeza kuwa pamoja na kuwa OR – TAMISEMI ni Wizara kubwa, kazi yake ya kuiongoza itakuwa rahisi endapo viongozi na watumishi wa wizara hiyo watafanya kazi kwa bidii, weledi na ushirikiano mkubwa huku akionesha kuwa hatokubali mtu yeyote kumrudisha nyuma katika kusimamia utekelezaji wa kazi katika ofisi hiyo.

“Naelewa TAMISEMI ni Wizara kubwa na inawagusa wananchi moja kwa moja kupitia Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serilai za Mitaa. Hivyo, ninaamini kuwa tukiwa na ushirikiano mzuri kazi itakuwa rahisi, lakini kama kiongozi akisema hili wengine wanasema lile kazi itakuwa ngumu na hatutafikia malengo na mimi sitakubali kurudishwa nyuma,” alisema.

Aliendelea kueleza kuwa anamshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumwamini na kumteua kuwa Mbunge na hatimaye Waziri katika Wizara hiyo huku akieleza kuwa ana uzoefu katika nafasi ya uwaziri ambapo ameongoza Wizara mbalimbli na hivyo atatumia uzoefu huo kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imedhamiria kuboresha maisha ya wananchi.

Awali, Waziri wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Innocent Basungwa alimueleza Waziri Kairuki kuwa OR – TAMISEMI ina viongozi na watumishi wazuri ambao alifanya nao kazi kwa ushirikiano mkubwa katika kipindi chote alichokuwa Waziri wa OR – TAMISEMI na hivyo anaamini kuwa ushirikiano huo utaendelea kwa Waziri Kairuki.

Bashungwa aliwashukuru watumishi wote wa OR – TAMISEMI kwa kufanya nae kazi vizuri ambapo alisema utendaji mzuri wa watumishi hao ndio ambao umefanya Rais Samia Suluhu Hassan aendelee kumwamini na kuamua kumteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

“Ninawashukuru sana watumishi wote kwa ushirikiano mlionipa katika kipindi chote nilichokuwa hapa. Kazi nzuri mliyoifanya ndiyo iliyofanya na mimi nionekane kuwa ninafanya vizuri. Ninamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuona bado ninafaa kuendelea kumsaidia katika Serikali yake. Ninawaomba ushirikiano na upendo mlionipa mumpatie pia Waziri Kairuki ili aweze kufanya kazi yake vizuri,” alisema Bashungwa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa OR – TAMISEMI, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya OR – TAMISEMI pamoja na watumishi wa Ofisi hiyo.