NKM TAMISEMI AWATAKA MAKATIBU WASAIDIZI TSC KUTOA ELIMU KWA WALIMU KUZUIA UKIUKAJI WA MAADILI YA KAZI

05 Mar, 2025
NKM TAMISEMI AWATAKA MAKATIBU WASAIDIZI TSC KUTOA ELIMU KWA WALIMU KUZUIA UKIUKAJI WA MAADILI YA KAZI

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Bw. Atupele Mwambene amewataka Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kutoa elimu kwa walimu ili kuzuia kuingia katika ukiukaji maadili ya kazi ya ualimu jambo linalosababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kupewa adhabu mbalimbali ikiwemo kufukuzwa kazi.

Ametoa kauli hiyo tarehe 4 Machi, 2024 wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa za Walimu kwa Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu Ngazi ya Wilaya yaliyofanyika katika Chuo cha Utumishi wa Umma mkoani Tabora.

Alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ya siku tatu ni kuwajengea uwezo Makatibu Wasaidizi wa Tume Ngazi ya Wilaya na Maafisa wa Tume ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aliongeza kuwa TSC ipo kwa ajili ya kusaidia walimu kupata uelewa juu ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayohusu utumishi wao hivyo, inapaswa kutoa elimu mara kwa mara badala ya kusubiri matatizo yatokee kwa walimu ndio waanze kutoa elimu.

“Tume ni chombo Mahususi kwa ajili ya kushughulika na masuala ya utumishi wa walimu, hivyo mtambue na kutekeleza kikamifu eneo la kutoa elimu kwa walimu, tuwe walezi bora kwa walimu hatupaswi kufurahia kufukuza kazi walimu,” alisisitiza.

Bw. Mwambene alisema kuwa Miongozo iliyoandaliwa ina lengo la kuweka kinga zaidi ya kuzuia ukiukwaji wa maadili ya Utumishi wa Walimu na Utumishi wa Uumma miongoni kwa walimu ili isaidie kuongeza tija katika kutoa huduma bora kwa wanafunzi.

Awali Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina Nkwama alisema kuwa TSC kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais TAMISEMI inatekeleza Programu ya miaka minne (2023/24 hadi 2026/27) ya uboreshaji wa Kada ya Ualimu (Teachers’ Support Programme -TSP).

Alisema kuwa Tume inatekeleza afua zinazosaidia kutoa motisha na uwajibikaji kwa walimu lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa ajili ya kuleta mageuzi katika sekta ya elimu nchini.

Mwl. Paulina alisema kuwa katika utekelezaji wa mradi Tume ya Utumishi wa Walimu ina jukumu la kuandaa na kusambaza Mwongozo wa Mafunzo Elekezi kwa walimu wanaoajiwa upya katika Utumishi wa Umma huku akiongeza kuwa linalotekelezwa ni kuendesha mafunzo kwa Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuhusu uendeshaji wa mashauri ya nidhamu na Rufaa kwa walimu.

Aidha, Mwl. Paulina alitaja mada zitakazofundishwa kwa Makatibu Wasaidizi hao ni pamoja na utaratibu wa kusimamia masuala ya nidhamu kwa walimu, mchakato wa kuendesha mashauri ya nidhamu na rufaa na kushughulikia masuala ya nidhamu yasiyo ya jinai. 

Mafunzo hayo ya siku tatu yameshirikisha Makatibu Wasaidizi wapatao 139 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.