PRO. MURUKE AWATAKA WATUMISHI TSC KUONGEZA NGUVU KUTOA ELIMU KWA WALIMU KUZUIA UKIUKWAJI WA MAADILI

Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wametakiwa kufanya juhudi katika kutoa elimu kwa walimu ili kuwaepusha kukiuka maadili ya kazi ya ualimu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 5 Mei, 2025 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Prof. Masoud Hadi Muruke wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya usimamizi wa mashauri ya nidhamu na rufaa za walimu kwa Maafisa wa Tume hiyo.
Alieleza kuwa lengo la TSC ni kuhakikisha walimu wanatekeleza majukumu yao ya kufundisha wanafunzi kwa kuzingatia maadili ya kazi hiyo, hivyo aliwataka maafisa hao kujikita katika kuzuia ukiukaji wa maadili kwa kutoa elimu badala ya kusubiri wakosee ili wawachukulie hatua za kinidhamu.
Alisema kuwa kuwepo kwa mashauri mengi ya nidhamu siyo sifa njema ya kuonesha kuwa ofisi inatekekeleza majukumu yake ipasavyo bali kazi inayohitajika ni kuhakikisha kuwa kila mwalimu anazingatia sheria, kanuni na taratibu na hivyo hakuna mashauri yanayojitokeza.
“Sio sifa nzuri kufukuza kazi walimu bali ni muhimu kutoa elimu kwa kuwatembelea mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wa kujua Sheria, Kanuni na Taratibu zinazohusu Utumishi wa Walimu na Utumishi wa Umma na kuzizingatia katika utendaji wao wa kazi,” alisisitiza.
Pamoja na hayo, Prof. Muruke alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa maafisa wa Tume kwani yatawajengea uelewa katika kushughulikia mashauri ya nidhamu na rufaa za walimu na hivyo kuwezesha kuzingatiwa kwa misingi ya haki katika kutoa uamuzi.
Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina Nkwama alisema kuwa chimbuko la mafunzo hayo ni kuondoa dosari za kutoizngatiwa kikamilifu kwa taratibu wakati wa kushughulikia mashauri nidhamu jambo linalosababisha rufaa za walimu zinazokatwa Tume Makao Makuu kurudishwa ili mashauri yaanzishwe upya kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Aliongeza kuwa rufaa kurudishwa ili mashauri yaanzishwe upya siyo tu kwamba inasababisha kucheleweshwa kwa haki bali inaisababishia hasara Serikali, hivyo aliwataka washiriki hao kuzingatia mafunzo ili watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi waongeze ufanisi wa utendaji kazi.
“Matarajio yetu ni kwamba baada ya mafunzo haya mtakwenda kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi zaidi. Tunatarajia kwamba hakuna rufaa itakayorudishwa ili shauri lianzishwe upya kwa kuwa taratibu hazikuzingatiwa,” alisema Mwl. Nkwama.
Katika hatua nyingine, Katibu huyo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake anazofanya katika kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuwezesha watumishi wa Tume kupata mafunzo hayo muhimu.
Awali, akitoa neno la utangulizi Mkuu wa Chuo na Mtengaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Ernest Francis Mabonesho alisema kuwa uhai wa taifa unategemea watumishi wenye weledi na mtazamo chanya kwa Serikali yao.
Alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu kwani yatawawezesha kuwa na uelewa wa kutosha katika kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu na hivyo kusaidia sekta ya elimu kuendelea kupiga hatua kimaendeleo.
Mafunzo hayo yanayoendeshwa chini ya ufadhili wa Programu ya kuboresha kada ya ualimu (GPE TSP) na kuendeshwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yamewahusisha Maafisa wa TSC Makao Makuu na wengine kutoka Ofisi za Wilaya za Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Morogoro, Songwe na Iringa.