PROF. MURUKE AKABIDHI MWONGOZO KWA MAKAMISHNA WA TUME

• Mwongozo huo unalenga kuwajengea uelewa walimu wapya kuhusu sheria, kanuni, taratibu na miongozo utumishi wao.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Masoud Hadi Muruke, tarehe 19 Agosti 2025 amekabidhi nakala za Kitabu cha Mwongozo wa Mafunzo Elekezi kwa Walimu Wapya Wanaoajiriwa Katika Utumishi wa Umma Tanzania Bara kwa Katibu na Makamishna wa Tume jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Muruke alisema mwongozo huo ni nyenzo muhimu ya kitaaluma na kiutumishi kwa walimu wapya, ili kuhakikisha wanazingatia miiko, maadili na taratibu za kazi yao mara baada ya kuajiriwa.
“Mwongozo huu umeandaliwa mahsusi na Tume ya Utumishi wa Walimu kwa lengo la kuwajengea uelewa walimu wapya kuhusu sheria, kanuni na miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma. Tunataka mwalimu mpya aingie kazini akiwa na mwongozo sahihi wa namna ya kutekeleza wajibu wake kwa nidhamu na uadilifu,” alisisitiza Prof. Muruke.
Mwongozo huo unafafanua kwa kina masuala ya haki na wajibu wa watumishi wa umma, mbinu bora za utendaji kazi, utunzaji wa kumbukumbu, na misingi ya utoaji wa huduma bora kwa wanafunzi na jamii. Pia unaeleza hatua za kinidhamu, taratibu za kupanda vyeo, pamoja na wajibu wa walimu katika kudumisha maadili na heshima ya taaluma ya ualimu.
Kwa mujibu wa Tume, lengo kuu la mwongozo huu ni kuhakikisha walimu wapya wanaingia kazini wakiwa na maarifa sahihi yanayowawezesha kutoa mchango bora katika kuimarisha sekta ya elimu na kufanikisha malengo ya kitaifa na kimataifa ya maendeleo ya elimu.
Taratibu za kusambaza mwongozo huo shuleni zinaendelea, na tayari unapatikana kupitia tovuti ya Tume: www.tsc.go.tz. Ni matarajio ya Tume kuwa mwongozo huu utakuwa dira ya walimu wapya katika kujenga nidhamu, uadilifu na ari ya kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya taifa.