PROF. MURUKE AWAPONGEZA WATUMISHI WA TSC WILAYA YA MOROGORO KWA KUTOA HUDUMA BORA KWA WALIMU
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Masoud Muruke tarehe 27 Agosti, 2024 ametembelea Ofisi za TSC Wilaya ya Morogoro na kuwapongeza watumishi wa Wilaya hiyo kwa namna wanavyotekeleza majykumu yao katika kutoa huduama kwa walimu.
Akitoka pongezi kwa Watumishi wa TSC wa Wilaya hiyo, Prof. Muruke alisma kuwa licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili ofisi hiyo, watumishi hao wameendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii, weledi na uzalendo na hivyo kufanya walimu wa Wilaya hiyo kuendelea kupata huduma bora.
Pamoja na pongezi hizo, Mwenyekiti huyo aliwataka watumishi hao kuendelea kutoa huduma bora kwa walimu ambao ni watumishi muhimu katika kuzalisha kada mbalimbali ambazo zinahitaji kwa maendeleo ya Taifa.
Prof. Muruke alisema kuwa alipokuwa ziarani Mkoani Dar es Salaam alifurahishwa na uchapakazi mzuri aliuona kwa Watumishi wa Tume wa wilaya za Mkoa huo na kuwataka kuendelea kutoa huduma bora licha ya kuwa na changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo uhaba wa miundombinu ya ofisi.
Aidha, Mwenyekiti aliitaka Menejimenti ya TSC kuhakikisha inaendelea kuboresha mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa Ofisi zake za wilaya kwani zenyewe ndio shina la kuleta mafanikio katika utekelezaji wa majukumu ya Tume.
Prof. Muruke aliongeza kuwa ni vema kuimarisha Ofisi za Wilaya ikiwemo kuwa na mazingira mazuri ya kuhifadhia nyaraka ambapo wakati mwingine zinatumika katika utoaji maamuzi ya masuala mbalimbali yanayohusu utumishi wa walimu.
“Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) inagusa sehemu kubwa ya utumishi wa walimu ikiwemo ajira, maendeleo ya walimu na inatoa maamuzi yanayohusu nidhamu za walimu, hivyo ni vyema tuhakikishe tunaweka mazingira mazuri ya katika ofisi hizi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi,” alisema.
Naye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama amewataka Watumishi wa Tume wilayani Morogoro kuhakikisha wanakwenda kutoa huduma kwa walimu katika maeneo yote ya Wilaya hiyo yakiwemo maeneo ya pembezoni kama Mvuha na Matombo.
Alisema kuwa maeneo ya Mvuha na Matombo yako mbali na ofisi za TSC, hivyo ni vyema kwa watumishi wa Tume kuweka utaratibu wa kupangiana zamu (rotation) ya kuwafikishia huduma walimu katika maeneo hayo.