SERIKALI INAFANYA JITIHADA KUBWA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WALIMU: NAIBU WAZIRI NDEJEMBI

14 Mar, 2023
SERIKALI INAFANYA JITIHADA KUBWA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WALIMU: NAIBU WAZIRI NDEJEMBI

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Serikali inafanya jitihada kubwa kuleta mageuzi katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuondoa kero na malalamiko mbalimbali yanayowakabili walimu na kuboresha mazingira ya kufundishia ili walimu watekeleze majukumu yao katika mazingira ya amani na utulivu.

Naibu Waziri ametoa kauli hiyo Machi 9, 2023 alipokutana na Menejimenti ya TSC ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika Tume hiyo tangu alipoteuliwa kushika nafasi ya Naibu Waziri OR – TAMISEMi hivi karibuni ambapo amesema dhamira ya serikali ni kuona walimu wote wanatatuliwa kero zao ili watekeleze majukumu yao kwa amani na utulivu.

Amesema kutokana na juhudi hizo za kuboresha mazingira ya walimu, ni muhimu kwa TSC kuendelea kuhakikisha walimu wanapata huduma bora ili waongeze ari katika kuhudumia wanafunzi kwa kuwa walimu wasipokuwa na moyo wa kufundisha Taifa litarudi nyuma kimaendeleo.

“Sote ni mashuhuda kuwa Serikali inafanya kazi kubwa katika kuhakikisha walimu wanatekeleza wajibu wao wakiwa katika mazingira mazuri. Ukiangalia katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia zile kero kubwa za walimu ikiwemo kutopandishwa madaraja amezimaliza. Hivyo, TSC kama chombo kinachosimamia utumishi wa walimu ni lazima muendelee kuongeza juhudi katika kutatua changomoto zilizobaki,” amesema Mhe. Ndejembi.

Pamoja na hayo, Kiongozi huyo amesema Rais Samia anatambua umuhimu na kazi kubwa inayofanywa na Tume hiyo kwa walimu, ndiyo maana ameruhusu miradi ya ujenzi wa jengo la Ofisi, ujenzi wa Mfumo wa kielektoniki wa kurahisisha utoaji huduma kwa walimu na miradi mingine ya wadau maendeleo kuisaidia kufanyika ili kuifanya TSC iimarike na kushughulikia walimu kwa ufanisi zaidi.

Akihitimisha hotuba yake fupi, Mhe. Ndejembi amesema kuwa atafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na TSC na kueleza kuwa kwake milango iko wazi muda wote kwa kiongozi anayehitaji kuonana nae kwa lengo la kushauriana masuala mbalimbali kwa ajili ya maslahi ya walimu.

Akimkaribisha Naibu Waziri huyo ili azungumze na Menejimenti ya Tume hiyo, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama ameeleza kuwa Tume hiyo inatekeleza miradi miwili kwa fedha za ndani na mradi wa BOOST unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa fedha za nje.

Akifafanua miradi hiyo Nkwama alisema, kupitia fedha za ndani TSC inatekeleza ujenzi wa jengo lake la Utawala la Ofisi ya Makao Makuu ambapo shughuli za ujenzi zinaendelea kupitia kwa mkandarasi SUMA JKT.

Amemweleza Naibu waziri huyo kuwa mradi mwingine ni Ujenzi wa Mfumo wa Kielektroniki ujulikanao kama Teachers’ Service Commission Management Information System (TSC-MIS) ambao umekamilika katika awamu ya kwanza huku ukijumuisha moduli sita ambazo zinajumuisha Usimamizi wa Mashauri, Usimamizi wa Rufaa, Msaada kwa Wateja na Malalamiko, Uratibu wa Wageni, Ajira na Usajili pamoja na Usimamizi wa Mafao na Mirathi.

Akizungumzia mradi wa BOOST, Mwl. Nkwama amesema katika kipindi cha nusu mwaka (Julai – Desemba, 2022) TSC ilipokea fedha za mradi huo kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi kiasi cha shilingi 633,002,856 kati ya shilingi 3,416,853,760 zilizoidhinishwa kwa ajili ya TSC kwa mwaka wa kwanza (2022/2023) wa utekelezaji wa mradi. 

“Kwa mwaka huu mradi wa BOOST unawezesha kutekeleza kazi mbalimbali ikiwemo; Kufanya mapitio ya Kanuni za Maadili na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu, kununua magari 15, laptops 159 na vifaa vingine vya TEHAMA pamoja na kufanya mapitio na kuhuisha Sheria zinazosimamia Utumishi wa Mwalimu kwa ajili ya kuandaa Sera ya kitaifa ya Mwalimu,” amesema.

Nkwama amehitimisha kwa kumshukuru Rais Samia kwa jitihada zake katika kuwahudumia walimu pamoja Ofisi ya Rais Tamisemi kwa ushirikiano wanauonesha kwa TSC katika utekelezaji wa majukumu ya utumishi wa walimu.