SERIKALI KUENDELEA KUONGEZA NGUVU KATIKA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA WALIMU

16 Feb, 2024
SERIKALI KUENDELEA KUONGEZA NGUVU KATIKA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA WALIMU

Serikali imesisitiza kuendelea kuweka nguvu kwenye matumizi ya teknolojia katika kutoa elimu shuleni ikiwa ni moja ya njia za kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu nchini.

Hayo yamesemwa Februari 12, 2024 na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Dkt. Charles Msonde wakati alipotembelewa na ujumbe wa wataalamu kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Serikali ya Mapindinduzi ya Zanzibar ambao wamefanya ziara Tume ya Utumishi wa Walimu kwa lengo la kujifunza namna Tume hiyo inavyotekeleza majukumu yake.

Dkt. Msonde alisema Serikali chini ya Utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada mbalimbali za kuboresha elimu ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu kama inavyohitajika.

“Kwa sasa tumeanza majaribio ya matumizi ya teknolojia ya ufundishaji inayowezesha Mwalimu kutoka kituo kimoja kufundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja wakiwa katika maeneo mbalimbali. Tumeanza majaribio haya katika Mikoa miwili ya Pwani na Dodoma na kwa kweli matokeo yake ni mazuri na wanafunzi wanafurahia,” alisema Dkt, Msonde.

Aliongeza kuwa, “kupitia teknolojia hiyo mwalimu anaona wanafunzi wake wote katika maeneo mbalimbali, anaweza kuuliza swali na mwanafunzi akanyoosha mkono na kujibu, yaani ni kama vile mwalimu yupo hapo hapo.”
 

Naibu Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa mbali na mfumo huo kurahisisha utendaji kazi kwa walimu, ni moja ya njia za kukabiliana na upungufu wa walimu hususan wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Ameongeza kuwa katika kuendeleza jitihada hizo, Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) tayari ameagiza kutengwa kwa bajeti ili kuwezesha upatikanaji wa angalau darasa moja kwa kila Mkoa na kila Halmashauri katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Pamoja na hayo, Dkt. Msonde alieleza kuwa TSC imeendelea kusimamia masuala ya utumishi wa walimu kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kusimamia ajira, maadili na maendeleo ya walimu ambapo hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ili kumaliza malalamiko ya walimu.

“Kama mna mpango wa kuanzisha chombo cha kushughulikia masuala ya walimu kama TSC, ninaamini mtapata mengi ya kujifunza na hivyo mtapata mwanga mzuri wa kuanzisha chombo kitakachosaidia upatikanaji wa huduma kwa walimu,” alisema Dkt. Msonde. 

Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe huo ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Bi. Mtumwa Iddi Hamad alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar ndiyo inayoshughulika moja kwa moja na usimamizi wa walimu kitu ambacho kinaleta changamoto katika usimamizi stahiki kwa walimu.

“Kutokana na hali hiyo Serikali ya Zanzibar inakusudia kuanzisha chombo maalum cha kushughulikia masuala ya walimu, hivyo tumekuja kujifunza kwa TSC ili kupata uzoefu wa namna inavyosimamia walimu huku Tanzania Bara,” alisema Mkurugenzi huyo.