SERIKALI YA KUAJIRI WATUMISHI 21,200 KADA YA UALIMU, AFYA

20 Apr, 2023
SERIKALI YA KUAJIRI WATUMISHI 21,200 KADA YA UALIMU, AFYA

Serikali imetangaza ajira za Watumishi wa Kada za Afya 8,070 kwa ajili ya Hospitali za Halmashauri, Vituo vya Afya na Zahanati pamoja na Ualimu 13,130 wa Shule za Msingi na Sekondari watakaofanya kazi chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Tangazo hilo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Jasmine Kairuki katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 12 Aprili, 2023 jijini Dodoma ambapo alisistiza kuwa waombaji wa ajira hizo  wanatakiwa kutuma maombi kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi cha ajira.tamisemi.go.tz.

“Wahitimu kutoka kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Afya vinavyotambuliwa na Serikali wanatangaziwa kutuma maombi ya kazi kuanzia tarehe 12 - 25 Aprili, 2023. Nafasi za ajira zilizopo ni kwa wahitimu wa Astashahada (Certificate), Stashahada (Diploma) na Shahada (Degree),” alisema Kairuki.

Akizungumzia kuhusu ajira za walimu Waziri Kairuki alisema kuwa tangazo hilo linawahusu wahitimu wa Kozi za Ualimu kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2022 huku akiongeza kuwa waombaji waliowahi kutuma maombi yao awali kupitia mfumo wa maombi ya ajira watahitajika kuhuisha taaarifa zao kwenye mfumo huo.

Alieleza kuwa nafasi za ualimu wa shule za msingi ninazohitajika kuombwa ni Mwalimu Daraja la III A mwenye Astashahada ya Ualimu Elimu ya Msingi, Elimu ya Michezo, Elimu Maalum na Elimu ya Awali (certificate in primary education); Mwalimu Daraja la IIIB awe na stashahada ya ualimu (diploma) waliosomea elimu ya Msingi; pamoja na Mwalimu Daraja la IIIC inayohitaji mwombaji mwenye shahada ya Ualimu kwa Elimu ya Awali.

“Nafasi za ualimu wa shule za Sekondari ni Mwalimu Daraja la III B inayohitaji mwaombaji awe mwenye Stashahada (Diploma) ya Ualimu aliyesomea Elimu Maalum kwa masomo ya English Language, Literature in English, Biology, Chemistry, Physics na Mathematics; Mwalimu Daraja la III C awe mwenye Shahada ya Ualimu aliyesomea Elimu Maalum kwa  masomo  ya  English  Language, Literature in English, Biology, Chemistry, Physics na Mathematics pamoja na Mwalimu Daraja la III B mwenye Stashahada ya Ualimu wa somo la English Language, Literature in English, Biology, Chemistry, Physics na Basic Mathematics,” alisema Waziri Kairuki.

Aliendelea kueleza nafasi zingine za walimu watakaoajiriwa kwa upande wa  shule za sekondari kuwa ni Mwalimu Daraja la III C ambapo mwombaji anatakiwa kuwa na Shahada ya Ualimu wa somo la English Language, Literature in English, Biology, Chemistry, Physics na Basic Mathematics pamoja na  Fundi Sanifu wa Maabara ambaye napaswa kuwa na Stashahada ya Ufundi Sanifu Maabara au Stashahada ya Sayansi na Teknolojia ya Maabara.

Kielezea sifa za jumla, Waziri Kairuki alisema mwombaji alazi awe raia wa Tanzania mwenye umri usiozidi miaka 45; awe na vyeti kamili vya mafunzo ya fani aliyosomea (Cheti cha Kidato cha Nne, Sita, Taaluma na usajili kamili (Full Registration) au Leseni hai ya kufanya kazi ya taaluma husika); asiwe Mwajiriwa wa Serikali au Mwajiriwa wa Hospitali za Mashirika ya Dini ambaye mshahara wake unalipwa na Serikali; awe hajawahi kufukuzwa, kuacha kazi au kustaafishwa katika Utumishi wa Umma; awe na Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA); na  aambatishe nakala ya cheti cha kuzaliwa.

Waombaji walioajiriwa kwa mkataba wa ajira kutoka kwa Wadau wa Maendeleo katika Sekta ya Afya wanatakiwa kuambatisha nakala za mkataba na barua za uthibitisho kutoka kwa Wakurugenzi wa Halmashauri husika. Pia, waombaji wenye Ulemavu na sifa zilizoainishwa watume maombi yao pia kupitia mfumo. Aidha, maombi yao yaeleze aina ya ulemavu alionao na kuambatisha picha na uthibitisho wa daktari kutoka katika hospitali za Serikali,” Waziri alisisitiza.

Pamoja na hayo, Waziri alielekeza kuwa waombaji wote wawe tayari kufanya kazi katika Halmashauri/Vituo watakavyopangiwa; wawe tayari kufanya kazi na Mashirika au Taasisi zilizoingia Ubia na Serikali; baada ya kupangiwa  kituo  cha  kazi, hakutakuwa  na  nafasi  ya kubadilishiwa kituo cha kazi; waombaji wote wahakikishe wanajaza taarifa zao na kuambatisha nyaraka zote muhimu kwenye mfumo.

Dirisha la kupokea maombi hayo lilifungwa tarehe 25 Aprili, 2023 saa 05:59 usiku ambapo taratibu zingine za ukamilishaji wa ajira hizo zinaendelea.