SILINDE AITAKA TSC KUTUMIA VIZURI FEDHA ZA MRADI WA BOOST

25 Jan, 2023
SILINDE AITAKA TSC KUTUMIA VIZURI FEDHA ZA MRADI WA BOOST

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Mhe. David Silinde ameitaka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuhakikisha inatumia vizuri fedha za Miradi wa BOOST ili ziweze kuleta tija katika maendeleo ya utumishi wa walimu nchini.

Silinde ameyasema hayo Januari 24, 2023 mjini Morogroro kwa niaba ya Waziri wa OR – TAMISEMI wakati akizindua Kitabu cha Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu kilichoandaliwa na TSC kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa BOOST ambapo uzinduzi huo umeambatana na Kikao kazi cha siku nne kinachowakutanisha Kaimu Katibu Wasaidizi wa TSC kutoka Wilaya zote Tanzania Bara.

Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu, amesisitiza sana fedha hizi za Mradi zitumike kwa Uadilifu na Uzalendo wa hali ya juu ili kuleta tija na kuwa na matokeo chanya ambayo yatawezesha nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo. Niwaombe sana wote tushirikiane vyema katika utekelezaji wa Mradi huu ili kuleta ufanisi uliokusudiwa katika sekta ya elimu. Niwasihi kutokubadilisha matumizi ya fedha za Mradi kinyume cha shughuli zilizopangwa,” amesema Naibu Waziri Silinde.

Akizungumzia kuhusu Kitabu hicho, Naibu Waziri Silinde amesema kuwa, kutokana na kuwepo kwa mabadiliko ya Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu, Utandawazi na ongezeko la idadi ya Walimu ni wakati sahihi kwa TSC kufanya mapitio na kutoa ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendeji Kazi katika Utumishi wa Walimu unaoendana na mabadiliko hayo.

Ameongeza kuwa ili kutimiza malengo ya kuwa na Shule Salama ni lazima kuhakikisha kuwa kila mwalimu anatambua na kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia Maadili ya kazi yake ikiwa ni pamoja na kumlea mwanafunzi kimwili, kiroho, kiakili, kisaikolojia na kijamii pamoja na kuwajibika katika taaluma yake, kwa mwajiri, jamii na Taifa kwa ujumla.

Kutokana umuhimu wa uzingatiaji wa Maadili, Naibu Waziri huyo ameiagiza TSC kuhakikisha Walimu wote nchini wanajengewa uwezo kuhusu Kanuni za Maadili ya Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu kwa kuzingatia ufafanuzi huo pamoja na kuandaa utaratibu wa kuwaelimisha walimu wapya wanapoajiriwa ili wanaposaini Mikataba ya Ajira wasaini pia kukubali kutekeleza Kanuni hizo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TSC, Prof. Willy Komba amesema kuwa ni muhimu kuhakikisha walimu wanasaidiwa kufahamu maadili ya kazi yao ili waweze kuandaa wanafunzi wenye weledi katika taaluma zao pamoja na kuwa na maadili mema katika jamii huku akisisitiza kuwa mwanafunzi asiyekuwa na maadili hata akifanya vizuri kitaaluma bado ni hasara kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Tunaahidi kuwa Tume itaendelea kutekeleza jukumu lake la kusimamia Utumishi na Maadili ya Walimu kwa lengo la kuhakikisha kuwa tunakuwa na Walimu wanaozingatia Maadili kwa ajili ya kuwalea Watoto wetu na hatimaye kuboresha elimu nchini,” alisema Prof. Komba.

Naye Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama amesema Tume ya Utumishi wa Walimu ni miongoni mwa Taasisi zinazotekeleza Mradi wa BOOST ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia na kupitia Mpango wa Shule Salama, Tume hiyo imewezeshwa kufanya Mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu kwa mujibu wa Kifungu cha 5 (j) cha Sheria Sura Na. 448.

Ameongeza kuwa kupitia mradi wa BOOST TSC imewezeshwa pia kufanya Mapitio ya Sheria na Kanuni zinazomhusu Mwalimu, Kununua vitendea kazi vikiwemo Kompyuta na Magari na kuwajengea uwezo Watumishi wa Tume hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.

Tume ina jukumu la msingi la kusimamia Maadili ya Kazi ya Ualimu chini ya Kifungu cha 5(c) cha Sheria Sura ya 448. Kifungu cha 5(j) cha Sheria hiyo kimeipa Tume jukumu la kutoa ufafanuzi kuhusu Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu. Hivyo, kutokana na matakwa ya Kanuni hizo na uwepo wa mabadiliko ya kisera, Sheria, Kanuni na Utandawazi, Tume iliona  umuhimu wa kurejea Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu na kuzitolea ufafanuzi,” amesema.

Ameongeza kuwa ufafanuzi kuhusu Kanuni hizo umeandaliwa na kuidhinishwa na Tume baada ya kupitia michakato mbalimbali ikiwemo ushiriki wa wadau kutoa maoni yao, uhariri wa nyaraka husika huku akieleza kuwa kazi ya kutafsiri ufafanuzi huo kwa lugha ya Kiingereza inaendelea.

Kwa mujibu wa Mwl. Nkwama, uzinduzi wa kitabu hicho ni hatua ya msingi ya kuhakikisha kuwa walimu wanazingatia maadili ya taaluma yao katika kutekeleza majukumu yao ili kutimiza azma ya Serikali ya kuwa naMpango wa Shule Salama.

Tume ina matarajio makubwa kwamba baada ya uwepo wa Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi wa Utumishi wa Walimu,  changamoto mbalimbali za  ukiukwaji wa Maadili ya Kazi ya Ualimu kwa walimu zitapungua au kuisha kabisa na hivyo kuifanya kazi ya Ualimu iendelee kuwa na hadhi yake inavyotakiwa” amesema Nkwama.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia elimu katika Mkoa huo, Mwl. Germana Mung'aho amesema kuwa Ufafanuzi huo ukizingatiwa vizuri walimu wote watakuwa na maadili mema na hivyo itaondoa dhana iliyojengeka kuwa walimu wa zamani ndio wenye maadili zaidi kuliko walimu wanaoajiriwa sasa.