TSC ARUMERU YAENDELEA KUTOA ELIMU KUHUSU UFAFANUZI WA MAADILI NA UTENDAJI KAZI KATIKA UTUMISHI WA WALIMU

31 Oct, 2023
TSC ARUMERU YAENDELEA KUTOA ELIMU KUHUSU UFAFANUZI WA MAADILI NA UTENDAJI KAZI KATIKA UTUMISHI WA WALIMU

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Arumeru imeendelea kutoa elimu kwa walimu kuhusu Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria Kanuni na Taratibu za utumishi huo.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Arumeru, Bi Zeituni Kinkwerema wakati wa ziara ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa TSC, Gerard Chami aliyoifanya wilayani hapo hivi karibuni.

Alisema pamoja na kuwafikia walimu moja kwa moja kwa kufanya ziara shuleni, Ofisi hiyo ilifanikiwa kuanzisha jukwaa la utoaji elimu juu ya Ufafanuzi huo kwa fungua kundi la WhatsApp ambapo walimu wengi wamepata elimu kwa njia hiyo.

Katika utekelezaji wa Utoaji Elimu kwa Walimu kuhusu ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu tuliweza kuwafikia Walimu na kuwaelimisha kwa kutengeneza kundi la Whatsapp ambalo tuliweka nakala laini ya kitabu cha Ufafanuzi wa kanuni za Utumishi wa Walimu. Walimu waliweza kupitia na kusoma maudhui yaliyoainishwa, pia walipata ufafaunuzi wa maswali mbalimbali yaliyokuwa yanawatatiza,” alisema.

Aliendelea kufafanua kuwa, “pia tuliweza kufanya ziara na kuzifikia baadhi ya Shule moja moja na baadae kuandaa ratiba ya kuwafikia Walimu na kuwaelimisha kwa kata. Shule zilizofikiwa katika Halmashauri ya Meru ni Kikatiti na Chemchem kwa Shule za Msingi na kwa Shule za Sekondari ni Akeri na Nasholi.

Aidha, Kinkwerema alieleza kuwa kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha ofisi yake ilitembelea Shule za Sekondari Mateves na Mringa, Pia utekelezaji umefanywa kwa kata katika kata ya Oldonyowasi yenye shule za Sekondari Namelok, Engutukoit, Losinoni Engedeko, Oldonyowasi na shule ya Msingi Oldonyowasi.

Pia, katika kata ya Bwawani tulikutana na Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari za Themi ya Simba, Bwawani, Songambele, Kigongoni na Olokii.”

Wilaya ya Arumeru ilipokea nakala za vitabu 120 vya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu kutoka TSC Makao Makuu kwa ajili ya kusambaza kwenye Halmashauri mbili ambavyo vililenga idara ya Elimu Msingi ambapo nakala 62 zimegawanywa katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru na nakala 58  ziligawanya katika Halmashauri ya Arusha.

Akizungumzia changamoto zonazoikabidli ofisi hiyo, Kinkwerema alieleza kuwa kuna upungufu wa vitendea kazi hususan kompyuta, uchakavu wa vyumba vya ofisi, upungufu wa watumishi wa kuhudumia walimu wa halmashauri mbili, pomoja na kukosekana kwa uhakika wa vyombo vya usafiri kwa ajili ya kufanya ziara shuleni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kutoka TSC Makao Makuu, Gerard   Chami alimpongeza Kaimu Katibu Msaidizi huyo kwa namna ofisi ya TSC Wilaya ya Arumeru inavyoendelea kutoa huduma kwa walimu huku akiahidi kuzifikisha changamoto zilizoibuliwa kwenye Menejimenti ya Tume kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi.

Wilaya ya Arumeru ina jumla ya shule za Msingi 296 ambapo katika idadi hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Meru in shule 116, na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha ina Shule 100. Wilaya ya Arumeru ina Shule za Sekondari 80, Meru Shule 45, Halmashauri ya Arusha Shule 35.

Aidha, Wilaya ya Arumeru ina jumla ya walimu 5,135 ambapo katika idadi hiyo Walimu 2,563 ni wa Halmashauri ya Meru na 2,572 ni wa Halmashauri ya Arusha.