TSC IMEFANIKIWA KUUNGANISHA MFUMO WA TSCMIS NA MIFUMO MINGINE MITATU

29 Aug, 2024
TSC IMEFANIKIWA KUUNGANISHA MFUMO WA TSCMIS NA MIFUMO MINGINE MITATU

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), imefanikiwa kuunganisha Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za walimu (TSCMIS) kwa ajili ya kusomana na Mifumo mingine ili iweze kubadilishana taarifa muhimu za walimu.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Takwimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Bi. Kainda Ndasa wakati akitoa mada kuhusu wasilisho la mfumo wa kielektroniki wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wapya wa Tume hiyo yaliyofanyika mjini Morogoro.

Alisema kuwa Mfumo wa TSCMIS hivi sasa umeunganishwa na Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi (e -watumishi), Mfumo wa Malipo ya Pensheni (Treasury Pensioners Payament System) na Mfumo wa Taarifa za Shule (School Information System) ambao utawezesha kujua mahudhurio, vipindi vinavyofundishwa na shule zenyewe.

Bi. Kainda alisema kuwa lengo la kuunganisha mifumo hiyo ni kutaka kubadilishana taarifa muhimu za walimu na kuboresha utendaji kazi, kuwa na taarifa sahihi katika kushughulikia masuala ya Ajira, Nidhamu, Rufaa na Mafao kwa walimu.

Bi. Kainda alisema kuwa Mfumo huo umesaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu katika kuwahudumia walimu kwa wakati na kwa ufanisi, kurahisisha mchakato wa kushughulikia mashauri ya Nidhamu na Rufaa za walimu kuanzia ngazi ya Shule, Wilaya hadi Makao Makuu na kurahisisha zoezi la kutoa namba za usajili kwa walimu (TSC Number).

Aliongeza kuwa Mfumo huo unawasaidia Walimu kupata huduma wakiwa katika vituo vya kazi na kuwaondolea usumbufu wa kufuata huduma katika Ofisi za Tume ngazi ya wilaya na upatikanaji wa taarifa kwa wakati na kwa usahihi.

Aidha, Bi. Kainda alisema kuwa Tume imepanga kuendelea na awamu ya tatu (3) ya ujenzi wa Mfumo wa TSCMIS pamoja na kufanya maboresho zaidi kulingana na mahitaji ya watumiaji hususan uchakataji wa taarifa kwa ajili ya maamuzi mbalimbali, kuendelea na usimikaji wa miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye Ofisi 103 za wilaya; na kutoa mafunzo kwa watumishi wa Tume katika Mikoa 15, Wakuu wa Shule na Maafisa TEHAMA wa Halmashauri.                                                

Katika hatua nyingine alisema kuwa Tume imetoa mafunzo kwa watumishi 65 kutoka Ofisi za Makao Makuu na Wilaya kwenye Mikoa minne (4); Dar es salaam, Dodoma, Mwanza, Iringa, Wilaya ya Kishapu na Morogoro katika awamu ya kwanza.

Aliongeza kuwa jumla ya watumishi 86 wa Ofisi za wilaya katika Mikoa saba (7), Katavi, Rukwa, Kigoma, Pwani, Singida, Simiyu na Mara wamepata mafunzo katika awamu ya pili kupitia ufadhili wa SHULEBORA.