TSC KUWEKA MIKAKATI MADHUBUTI KUFANYA VIZURI KWENYE MICHEZO

31 Oct, 2023
TSC KUWEKA MIKAKATI MADHUBUTI KUFANYA VIZURI KWENYE MICHEZO

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama amesema Tume hiyo inajipanga kimkakati katika michezo ili kufanya vizuri zaidi katika mashindao mbalimbali yanayofanyika.

Mwl. Nkwama ameyasema hayo Oktoba 13, 2023 mjini Iringa alipokutana na wachezaji wa timu ya TSC wanaoshiriki katika mashindano ya SHIMIWI kwa mwaka 2023 yanayofanyika katika viwanja mbalimbali mjini Iringa.

Amesema ni muhimu kuangalia michezo ambayo TSC inaweza kufanya vizuri na kuiwekea nguvu zaidi ili kuweza kutwaa makombe katika mashindano mbalimbali.

“Ninaamini tunaweza kufanya vizuri zaidi tukiwa na mikakati na maandalizi mazuri. Siyo lazima kuweka nguvu kwenye michezo yote, tuangalie michezo ambayo tuna wachezaji wazuri inayoweza kutuletea ushindi. Tukibainisha michezo hiyo, tunaiwekea mikakati na maandalizi mazuri na hatimaye tuweze kupata makombe mengi zaidi,” alisema Katibu huyo.

Katibu huyo aliwapa fursa wachezaji kueleza michezo wanayoona TSC inaweza kufanya vizuri zaidi ambapo walitaja kuwa ni Karata, bao, kurusha vishale (darts), kuendesha baiskeli, draft, netball, tufe na kuvuta kamba.

Baada ya kubainishwa michezo hiyo, Mwl. Nkwama aliwaelekeza viongozi wa michezo kuhakikisha wachezaji wanafanya mazoezi wakati wote badala ya kusubiri hadi yanapotokea mashindano.

“Pamoja na mazoezi, tunajipanga kutafuta fedha kwa kutafuta wadau ambao wanaweza kutusaidia ili tuimarishe timu zetu. Pia, tutatafuta vifaa vya michezo ili wachezaji wetu wavitumie wakati wa mazoezi,” alisema Mwl. Nkwama.

Katibu huyo, aliwapongeza wachezaji kwa kushiriki mashindano hayo na kudumisha nidhamu katika kipindi chote cha michezo hiyo.

“Nimefurahi kuwaona mmeshiriki vizuri na sisi TSC tumeonekana na tumeendelea kujitangaza. Pamoja na kushindana mmepata pia fursa ya kukutana na watumishi wenzenu kutoka maeneo mengine na mmebadilishana uzoefu na kupata marafiki wapya. Hongereni kwa ushindi katika mchezo wa Tufe na michezo mingine tuliyoshiriki,” amesema Nkwama.

Awali, akitoa taarifa ya ushiriki wa TSC katika mashindao ya SHIMIWI, Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo wa Tume hiyo, Gerard Chami alimweleza Katibu huyo kuwa timu ya TSC ilikuwa na jumla ya wachezaji 14 ambao walishiriki michezo ya kuvuta kamba, riadha, kurusha tufe, bao, karata, draft, kuendesha baiskeli na kurusha vishale.

“Katika mchezo wa kurusha tufe kwa upande wa wanawake tumeshika nafasi ya kwanza, mchezo wa bao na karata tulifika robo fainali. Tunashukuru wachezaji wote wamekuwa katika hali nzuri kiafya kwa muda wote ambao tumekuwa hapa Iringa,”alisema Chami.

Mashindano ya SHIMIWI yalianza Septemba 28, 2023 na kuhitimishwa Oktoba 14, 2023.