TSC MBIONI KUKAMILISHA MWONGOZO WA MAFUNZO ELEKEZI KWA WALIMU WAPYA KAZINI

22 Nov, 2024
TSC MBIONI KUKAMILISHA MWONGOZO WA MAFUNZO ELEKEZI KWA WALIMU WAPYA KAZINI

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeendesha kikao kazi cha kupitia rasimu ya Mwongozo wa Mafunzo Elekezi kwa Walimu wanaoajiriwa kwenye Utumishi wa Umma ili waweze kuzingatia masuala muhimu yanayohusu Utumishi wao.

Akifungua kikao kazi hicho kinachoendeshwa na TSC kupitia Mradi wa Global Partnership for Education (GPE) tarehe 21 Novemba, 2024 mjini Morogoro, Mwenyekiti wa Tume Prof. Maosud Hadi Muruke alisema kuwa maboresho ya mwongozo huo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya ya utumishi wa walimu nchini.

Alisisitiza kuwa mwongozo huo umeandaliwa ili kuondoa utofauti katika kuwaelekeza walimu wapya mara wanapoajiriwa kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma.

“Mwangozo umetoa maelekezo mahsusi kwa Walimu wapya kuhusu Misingi ya Utumishi wa Umma na Utumishi wa Walimu, haki na wajibu wao pamoja na miiko na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na taratibu zingine,” alisema.

Kwa upande wa Katibu wa Tume ya Utimishi wa Walimu, Mwl. Paulina Nkwama alisema kuwa mwongozo utawasaidia walimu wanaoajiriwa katika Utumishi wa Umma Tanzania bara kupata uelewa mzuri wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma kwa ujumla na hususani katika Utumishi wa Walimu.

Mwl. Paulina aliongeza walimu wataweza kufahamu haki, wajibu, maadili yanayoongoza Utumishi wa Umma na taaluma ya kada yao kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi na hivyo kuwa na Utumishi wa Umma wenye tija na utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Sanjari na hilo, Mwongozo huo unalenga kuwapatia walimu wapya taarifa za msingi kuhusu haki na wajibu wao kama watumishi wa umma, kuwawezesha kufahamu mbinu bora za kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuwasisitiza umuhimu wa kujitambua kama watumishi wanaowajibika kwa jamii.

Aidha, Mwl. Paulina alisema kuwa mwongozo unalenga kuwaelimisha walimu kuhusu taratibu za kupanda madaraja, taratibu na hatua mbalimbali za kinidhamu, na umuhimu wa kudumisha uadilifu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.