TSC YAADHIMISHA SIKU YA WALIMU DUNIANI KWA KUENDESHA KLINIKI YA KUTOA HUDUMA KWA WALIMU

03 Nov, 2024
TSC YAADHIMISHA SIKU YA WALIMU DUNIANI KWA KUENDESHA KLINIKI YA KUTOA HUDUMA KWA WALIMU

Katika kuadhimisha Siku ya Walimu Duniani, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) inaendesha Kliniki ya kutoa huduma kwa walimu na wadau mbalimbali inayofanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 5 hadi 11 Oktoba, 2024 katika Ofisi za TSC Makao Makuu jijini Dodoma.

 

Akizungumza na vyombo vya habari tarehe 5 Oktoba, 2024, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama alisema walimu wanakaribishwa kufika katika kliniki hiyo kupata elimu na kutatuliwa changamoto za kiutumishi zinazowakabili.

 

Alisema TSC ni mdau muhimu katika kuadhimisha Siku ya Walimu Duniani kwa kuwa kwa walimu walioajiriwa katika utumishi wa umma wanaofundisha kwenye shule za Msingi na Sekondari Tanzania Bara wanahudumiwa na Tume hiyo ambapo kwa sasa Tume inahudumia walimu 274,541 huku walimu 180,325 wakiwa ni wa shule za Msingi na 94,216 ni wa shule za Sekondari.

 

Akizungumzia namna Serikali kupitia TSC inavyoshughulikia maslahi ya walimu, Mwl. Nkwama alisema Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan jumla ya walimu 37,473 wameajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

 

‘‘Kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 walimu waliopandishwa vyeo ni 126,346, mwaka 2021/2022 walimu waliopandishwa vyeo ni 35,112, mwaka 2022/2023 ni 65,925 na mwaka 2023/2024 walipandishwa vyeo walimu 158,916. Aidha, katika kipindi hicho walimu 25,006 wamebadilishiwa vyeo baada ya kujiendeleza kielimu,” alisema.

 

Aliongeza kuwa Tume hiyo imefanya ziara shuleni kwa ajili ya kutoa elimu na ufafanuzi wa maadili katika utumishi wa walimu ili kuwawezesha kuelewa wajibu na haki zao kwa lengo la kuwaepusha walimu kufanya makosa yanayopelekea kuchukuliwa hatua za kinidhamu, ambapo jumla walimu 265,880 wa shule za msingi na sekondari walifikiwa.

 

Kwa mujibu wa Mwl. Nkwama, TSC imefanikiwa kujenga Mfumo wa kielektroniki wa TSCMIS-Teachers Service Commission Management Information System wenye lengo la kuboresha utendaji kazi katika kuwadumia walimu kwenye masuala ya Ajira na Maadili.

 

‘‘Serikali kupitia Mradi wa BOOST imeipatia Tume jumla ya magari 11 kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa walimu ngazi ya wilaya na Makao Makuu, kuwajengea uwezo jumla ya wajumbe 426 wa Kamati za Tume za Wilaya za Ajira, Upandishwaji vyeo na Nidhamu ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia utumishi wa walimu,” alisema Katibu huyo.

 

Aidha, Mwl. Nkwama alisema, TSC inatarajia kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakuu wa shule 3,066 ili kuwawezesha kusimamia masuala ya Maadili kwenye ngazi za shule kwa kuzingatia kuwa wao ni Mamlaka ya Nidhamu ngazi ya shule. Aidha, Tume imeandaa na kusambaza jumla ya vitabu 20,000 kwenye shule za Msingi Tanzania Bara kuhusu ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na  utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu.

 

‘‘Vilevile Tume kupitia Mradi wa SHULEBORA imefanikiwa kuandaa na kuchapisha vitabu 200 kuhusu ufafanuzi wa masuala muhimu yaliyomo katika Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 na Kanuni zake za mwaka 2016. Tume pia kwa kushirikiana na World Vision imefanikiwa kuandaa kitini cha kufundishia walimu wa shule za Msingi na Sekondari masuala ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya walimu,” alisema.

 

 Siku ya Walimu Duniani huadhimishwa tarehe 5 Oktoba ya kila mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya kupitishwa kwa Pendekezo la ILO/UNESCO mwaka 1966 kuhusu Hadhi ya Walimu lililoweka viwango vya Haki na Wajibu wa Walimu.

 

Pendekezo hilo huangazia viwango vya mafunzo ya Taaluma ya ualimu, Mafunzo kazini, Ajira pamoja na Masharti ya Kufundishia na Kujifunzia huku likitambua mchango wa Walimu katika kuboresha Elimu na kujadili maslahi yao.