TSC YAENDELEA KUHUDUMIA WATEJA KWENYE MAONESHO YA NANENANE JIJINI MBEYA

03 Aug, 2022
TSC YAENDELEA KUHUDUMIA WATEJA KWENYE MAONESHO YA NANENANE JIJINI MBEYA

Banda la Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) lililopo katika viwanja vya maonesho ya Nanenane jijini Mbeya limeendelea kupokea wateja kwa wingi wanaofika kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na TSC.

Miongoni mwa wateja waliotembelea banda hilo ni walimu ambao walitaka kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu huduma za kiutumishi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari za Serikali.

Miongoni mwa masuala yaliyoulizwa kwa upande wa huduma kwa walimu ni namna mchakato wa usajili wa walimu unavyofanyika, vigezo vinavyotumika kumthibitisha kazini mwalimu, taratibu za kupanda vyeo/madaraja, mchakato wa kubadilisha kazi/cheo baada ya mwalimu kujiendeleza kimasomo pamoja na hatua za kuzingatia pale mwalimu anapohitaji kustaafu kazi.

Vilevile, wateja walipata fursa ya kujua mchakato wa mashauri ya nidhamu yanavyofanyika kuanzia ngazi ya Shule, TSC Wilaya, TSC Makao Makuu pamoja na haki ya kukata Rufaa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale ambapo mwalimu hakuridhika na uamuzi wa rufaa yake unaofanywa na TSC Makao Makuu.

Pamoja na maelezo na ufafanuzi unaotolewa, wateja wanapatiwa vipeperushi vyenye maelezo zaidi kuhusu TSC na huduma zake ili waendelee kujisomea na kupata uelewa mpana wa haki na wajibu wa mwalimu ambaye ni Mtumishi wa Umma.