TSC YAENDESHA MAFUNZO YA PEPMIS KWA KAIMU KATIBU WASAIDIZI, YAGAWA LAPTOP 159

01 Dec, 2023
TSC YAENDESHA MAFUNZO YA PEPMIS KWA KAIMU KATIBU WASAIDIZI, YAGAWA LAPTOP 159

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeendesha mafunzo kuhusu matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (Public Employees Performance Management Information System (PEPMIS)) kwa Kaimu Katibu Wasaidizi wa TSC kutoka wilaya zote 139 za Tanzania Bara.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika Novemba 29, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma yalilenga kuwajengea uwezo watumishi hao ambao ni watekelezaji wa majukumu ya Tume katika ngazi ya wilaya.

Sambamba na mafunzo, Tume hiyo imetoa kompyuta mpakato (laptop) kwa kila Kaimu Katibu Msaidizi ili kuweza kurahisisha utendaji kazi wa kutoa huduma kwa walimu.

Akitoa maelezo wakati wa kufungua mafunzo hayo, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama aliwataka washiriki hao kuwa wasikivu ili waweze kupata uelewa wa kutumia mfumo huo kikamilifu kama inavyohitajika.

“Kulingana na umuhimu wa mafunzo haya, tumeona tuwaite wote hapa Dodoma ili mpate uelewa wa mfumo huu kwani utekelezaji wa majukumu ya Tume ngazi ya Wilaya unawategemea ninyi. Ni imani yangu kuwa baada ya mafunzo mtatekeleza kikamilifu yote mnayopaswa kufanya kupitia mfumo huu,” alisema Nkwama.

Akizungumzia huhusu vitendea kazi, Mwl. Nkwama aliwatakata watumishi hao kuvitumia vizuri kwa ajili ya kurahisiha utoa huduma kwa walimu huku akionya kuwa hatamvumilia mtumishi atakayekuwa mzembe katika utunzaji wa vifaa hivyo.

“Serikali kupitia mradi wa BOOST imetumia kiasi cha shilingi 375,000,000 kwa ajili ya kununua kompyuta mpakato 159 tulizowapatia. Hakuna tena sababu ya kutokamilisha kazi kwa kisingizio cha kutokuwa na kompyuta. Ninawasihi vifaa hivi tuvitunze na tuvitumie kwa malengo yaliyokusudiwa, hatutavumilia uzembe wa aina yoyote katika utunzaji na utumiaji wa vifaa hivi,” alisema Nkwama.

Kwa upande wa msimamizi wa mafunzo hayo ambaye pia Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi wa Umma kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Felister Emmanuel Shuli alisema mfumo wa PEPMIS utaleta uhalisia katika upimaji wa utendaji kazi tofauti na utaratibu uliokuwa unatumika awali, hivyo utaongeza kasi ya uwajibikaji kwa kila mtumishi.