TSC YAKUTANISHA WADAU KUTOA MAONI KATIKA KUANDAA MWONGOZO WA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA MASUALA YA NIDHAMU NA RUFAA KWA WALIMU

16 Jan, 2025
TSC YAKUTANISHA WADAU KUTOA MAONI KATIKA KUANDAA MWONGOZO WA MAFUNZO YA USIMAMIZI WA MASUALA YA NIDHAMU NA RUFAA KWA WALIMU

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeandaa kikao kazi kinachowakutanisha wadau wa elimu kwa lengo la kutoa maoni ya Rasimu ya Mwongozo wa Mafunzo ya Usimamizi wa Masuala ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu katika Utumishi wa umma.

Akifungua kikao hicho tarehe 15 Januari, 2025 mjini Morogoro, Mwenyekiti wa TSC, Prof. Masoud Hadi Muruke alisema lengo la Tume kuandaa Mwongozo huo ni kuwajengea uwezo watumishi wa Tume, Mamlaka za nidhamu na Wajumbe wa Tume kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika kushughulikia uendeshaji wa mashauri ya nidhamu na rufaa za walimu.

Prof. Muruke aliwataka wadau kutoa maoni kwa uhuru na weledi ili kuweza kuandaa mwongozo utakaosaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa mamlaka za Nidhamu na rufaa kwa walimu.

Aliongeza kuwa katika kuandaa mwongozo huo ushiriki wa wadau mbalimbali wa elimu ni jambo muhimu ili kuhakikisha mabo yote muhimu yanazingatiwa.

Aidha, Mwenyekiti huyo alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za dhati za kuiwezesha Tume kuwa sehemu ya mikakati ya Taifa katika kuinua kiwango cha elimu na kusimamia mazingira ya kazi ya walimu ili kuinua kiwango cha elimu kupitia ufundishaji na ujifunzaji.

“Natambua kwamba kuwepo kwetu hapa ni matokeo ya juhudi za Serikali anayoiongoza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kupitia ufadhili kutoka Global Partnership for Education (GPE), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikishirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, inatekeleza Programu ya miaka minne (2023/24 hadi 2026/27) ya Uboreshaji wa Kada ya Ualimu (Teacher Support Programme - TSP),” alisisitiza.

Awali akitoa maelezo ya utangulizi, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, inatekeleza Programu ya miaka minne (2023/24 hadi 2026/27) ya Uboreshaji wa Kada ya Ualimu (Teacher Support Programme - TSP).

Alisema kuwa lengo kuu la programu hiyo ni kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ili kuinua kiwango cha elimu nchini.

Mwl. Paulina alisema kuwa katika utekelezaji wa programu hiyo, Tume ya Utumishi wa Walimu ina jukumu la kutoa mafunzo kwa watumishi wa Tume na Makamishna kuhusu uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu.

Alisema kuwa kwa msingi huo, Tume ya Utumishi wa Walimu kupitia programu ya Uboreshaji wa Kada ya Ualimu (Teacher Support Programme - TSP) chini ya mradi wa  Global Partnership for Education (GPE), imeandaa rasimu ya Mwongozo wa Mafunzo ya Usimamizi wa Masuala ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu katika Utumishi wa Umma utakaoziwezesha mamlaka za nidhamu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Mwl. Paulina alisema mara baada baada ya mwongozo huo kukamilika mafunzo yatatolewa kwa wadau mbalimbali wanaohusika na usimamizi wa masuala ya nidhamu na rufaa za walimu ili kuwaongezea uelewa katika sheria, kanuni, na taratibu zinazotumika katika kuendesha masuala hayo.