TSC YAPONGEZWA KWA KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA KWA WALIMU

05 Aug, 2022
TSC YAPONGEZWA KWA KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA KWA WALIMU

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mhe. Dkt Julius Ningu ameipongeza Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwa kuendelea kusimamia ajira, maadili, maendeleo na maslahi mbalimbali ya walimu kitu ambacho kimesaidia kuleta utulivu kwa walimu nchini.

Mkuu huyo wa Wilaya ametoa pongezi hizo leo tarehe 5 Agosti, 2022 alipotembelea banda la TSC lililopo ndani ya Uwanja wa John Mwakangale katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Mbeya huku akieleza kuwa TSC ina wajibu wa kuhakikisha kero ndogondogo zinazowakabili walimu zinafanyiwa kazi ili waendelee kuwa na moyo wa kutumikia Taifa lao.

Aliongeza kuwa Sekta ya Elimu imeendelea kuimarika kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri unaofanywa na TSC katika kuwaelimisha walimu juu ya sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Walimu na matokeo ya jitihada hizo ni pamoja na kuendelea kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari nchini.