TSC YASHAURIWA KUELIMISHA WALIMU KUZUIA UKATILI NA UNYANYASAJI WA WATOTO

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeshauriwa kuongeza kasi katika kutoa elimu kwa walimu na wadau mbalimbali wa elimu ili kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji vikiwemo ubakaji, ulawiti, ushoga, vipigo na mauaji ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi wakiwa shuleni na nje ya shule.
Kauli hiyo imetolewa Februari 21, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Halima Dendego wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu cha wadau wa elimu kutoka Wilaya za Iringa na Mufindi ambacho kimeandaliwa na TSC kwa ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la World Vision Tanzania kinachofanyika mjini Iringa.
Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa ni muhimu kwa walimu kukumbushwa juu ya miiko na maadili ya kazi yao kwa kuwa vipo vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto vinavyofanywa na wanajamii wakiwemo baadhi ya walimu huku akisisitiza kuwa vitendo hivyo sio kwamba vinarudisha nyuma maendeleo ya elimu kwa watoto tu bali vinatishia ustawi na usalama wao.
Amefafanua kuwa takwimu za hivi karibuni za matukio ya unyanyasaji dhidi ya watoto, wanawake na wanaume zinaonesha kuwa katika Mkoa wa Iringa vitendo hivyo bado vipo na vinaendelea kufanyika kwa kiwango kikubwa na hivyo ni muhimu kuongeza kasi ya kuelimisha wadau wote ili jamii iishi kwa kuzingatia maadili yanayomwandaa mtoto kuwa raia mwadilifu na mwenye tija kwa taifa.
“Mkoa wetu sio kisiwa, upo kama mikoa mingine na suala la unyanyasaji bado lipo. Tukiangalia takwimu za hivi karibuni tuna matukio zaidi ya 2,600 ya unyanyasaji dhidi ya watoto, matukio zaidi ya 2,400 ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na kwa upande wa wanaume tuna matukio zaidi ya 154. Ukiyajumuisha haya yote mengine yamesababisha vifo, msongo wa mawazo au maumivu yasiyoweza kutibika. Mbaya zaidi ni pale unapokuta mwalimu aliyepewa dhamana ya kuwalea watoto katika maadili mema, naye ni miongoni mwa wale wanaotenda haya,” amesema Mhe. Dendego.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa katika kuboresha sekta ya elimu ambapo katika kipindi cha miezi sita (6) iliyopita Mkoa huo umepokea shilingi zaidi ya bilioni 5.5 kwa ajili ya kugharamia elimu bila malipo, shilingi zaidi ya bilioni 2.9 zimetumika kulipa madeni ya watumishi wengi wao wakiwa ni walimu huku shilingi zaidi ya bilioni 8 zikitumika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo kujenga vyumba vya madarasa, maabara na matundu ya vyoo.
“Jitihada hizi zinazofanywa na Mhe. Rais wetu hazitakuwa na maana endapo hatutaongeza jitihada za kusaidia watoto wetu wasiangamie kutokana na vitendo vya mmomonyoko wa maadali vinavyozidi kuongezeka. Hivyo, pamoja na kazi kubwa na nzuri mnayoifanya TSC, ninawashauri kuongeza jitihada kuwafikia walimu na wadau wengine kuwapa elimu na mbinu za kuwalinda watoto wetu,” amesema.
Hata hivyo, kiongozi huyo ameipongeza TSC kwa hatua inayoendelea kuchukua katika kuwafikia walimu kupitia kuandaa maadiko mbalimbali ya miradi kwa wadau wa maendeleo na kupata fedha za kutekeleza majukumu hayo huku akisema kuwa huo ndio mfano mzuri wa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuboresha elimu nchini.
“Ninaipongeza Menejienti ya TSC kwa ubunifu mlioutumia kwa kuandika andiko la mradi na kulipeleka na matunda yake ni haya tunayoyaona sasa kwamba World Vision Tanzania wamejitokeza kuwawezesha kifedha ili mfanye mafunzo haya muhimu. Ninawapongeza sana kwa kuona fursa hiyo na kuitumia, maeneo mengine unakuta watendaji wamekaa tu kusubiri fedha ya serikali ambazo hazitoshelezi kukidhi mahitaji yote,” amesema.
Aidha, Dendego amelipongeza shirika la World Vision Tanzania kutokana na jitihada zake za kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuimarisha ustawi wa watoto kwa kupambana na vitendo vya unyanyasaji na ukatili, kuimarisha usawa wa kijinsia pamoja na kuboresha uchumi wa wananchi katika maeneo mbalimbali.
“Ninawashukuru World Vision Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza shughuli mbalimbali zenye lengo la kukuza usawa wa kijinsia na kupinga kila aina ya ukatili na uonevu dhidi ya watoto. Ninaelewa kuwa, moja ya njia ya kukuza usawa huo wa kijinsia ni kuboresha mazingira ya kusomea na kujifunzia, ikiwa ni pamoja na kuongeza vyumba vya madarasa na madawati pamoja na kununua vitabu kwa ajili ya shule ili kuhakikisha watoto wa jinsia zote wanapata fursa ya kuendelezwa,” amesema.
Akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya Katibu wa TSC, Mwalimu Mkuu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu Makao Makuu, Romuli Rojas amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 TSC iliandaa andiko mradi linaloitwa ‘Enhansing Teachers’ Ethics and Professional Conduct in Primary and Secondary Schools’ (ETEP) ikiwa ni moja ya juhudi za kuwasiliana na wadau wa maendeleo ili kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuimarisha maadili ya walimu ili watoe huduma bora kwa wanafunzi.
Ameongeza kuwa Kikao Kazi hicho kinawahusisha washiriki 20 ambao ni Maofisa wa TSC, Wajumbe wa Kamati za Wilaya, Wadhibiti Ubora wa Shule, Maafisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya pamoja na Maafisa elimu wa Wilaya wote kutoka Wilaya za Iringa na Mufindi na kusema kuwa watakuwa wawezeshaji kwenye ngazi ya shule kwa utaratibu ambao wilaya husika itaupanga kwa kushirikiana na Shirika la World Vision Tanzania ili kufikisha elimu kwa walimu ngazi ya Shule na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Kata.
Kwa upande wa mwakilishi kutoka World Vision Tanzania, Zacharia Shigukulu amesema Shirika hilo limeingia makubaliano na Serikali ya namna ya kushiriki kwa pamoja katika kupambana na vitendo vya unyanyasaji wa watoto ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wadau ili kupiga vita vitendo hivyo kwa watoto na wanawake.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa World Vision Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa pamoja na Serikali katika kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji na ukatili kwa watoto. Huku kwetu Iringa vipo viashiria vingi vinavyoonesha kwamba wapo watu wanaojihusisha na vitendo hivyo. Lakini kwa bahati mbaya zaidi vimekwenda mpaka vimegusa walimu wetu ambao wanajukumu la kuwalea watoto,” amesema Zacharia.
Ameongeza kuwa, “kupitia mafunzo haya tuna amini kuwa elimu itakayotolewa itawafikia walengwa ili kupunguza na hatimaye kutokomeza vitendo hivi. Tunataka Taifa liendelee kwa kuwa na watoto wenye maadili mema, waliofundishwa vizuri na ambao hawajaathirika kisaikolojia ili tuwakuze vizuri na watakapokuwa watu wazima wakatekeleze majukumu yao vizuri kwa ajili ya kuleta maendeleo katika Taifa letu la Tanzania.”