TSC YATEMBELEA GEREZA LA WANAWAKE ISANGA NA KUTOA MSAADA

26 Jun, 2023
TSC YATEMBELEA GEREZA LA WANAWAKE ISANGA NA KUTOA MSAADA

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imefanya ziara katika Gereza la Wanawake Isanga lililopo jijini Dodoma na kutoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kusaidia jamii katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma inayofanyika tarehe 16 hadi 23 Juni kila mwaka.

 

Ziara hiyo iliyoongozwa na Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama imefanyika tarehe 22 Juni, 2023 ambapo amesema TSC imeona ni muhimu kufika katika gereza hilo na kutoa msaada kwa ajili ya kuwasaidia wanawake pamoja na watoto waliopo katika gereza hilo.

 

Nkwama amesema kwa mujibu wa maelekezo ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi, Taasisi zote za Umma zinapaswa kufanya mambo makuu mawili ambayo ni kutembelea watumishi ili kusikiliza kero na changamoto wanazokutana nazo katika mazingira yao ya kazi na kuona namna bora ya kuzitatua.

 

“Jambo la pili lililosisitizwa na Katibu Mkuu ni kutembelea taasisi mbalimbali zenye mahitaji na kufanya kitu kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji. Hivyo, tumeona tuje tutembelee hapa Gereza la Isanga na Mahsusi kuwaona wafungwa wa gereza la wanawake,” amesema Nkwama.

 

Ameongeza kuwa sababu ya kutembelea gereza hilo ni kumuenzi Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ni mwanamke lakini pia amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za mtoto wa kike ikiwemo kuruhusu wasichana wanaopata ujauzito kuendelea na masomo jambo ambalo huko nyuma watoto wengi walipoteza haki yao ya kuendelea na masomo baada ya kupata ujauzito.

 

“Sisi tunahudumia walimu wanaofundisha shule za msingi na sekondari za Serikali katika masuala ya Ajira, Maadili na Maendeleo yao. Rais wetu mpendwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kulegeza baadhi ya masharti yaliyokuwepo kule shuleni, ilikuwa mwanafunzi wa kike akipata ujauzito ndoto zake za kuendelea na shule zilikuwa zimeishia hapo, hasa wale waliotoka mazingira magumu ilikuwa ndo mwisho wao.”

 

“Huko nyuma tuliwapoteza wanawake wengi kwenye sekta hii ya elimu kwasababu tu wamepata ujauzito. Lakini baada ya Rais Samia kuingia madarakani akasema wanafunzi wote waliopata ujauzito wakishajifungua watoto wapewe haki yao ya kunyonyeshwa na baada ya miaka miwili warudi shuleni kuendelea na masomo. Kwa kweli tunampongeza Rais wetu na katika kuenzi jitahada zake tumeona ni muhimu tuje kwenye gereza hili kuwatembelea wafungwa wanawake,” amesema Katibu huyo.

 

Baadhi ya Misaada iliyotolewa ni blanketi, kandambili, soksi za mtoto mchanga, sweta za watoto, miswaki, dawa ya meno, mafuta ya kupaka, sabuni ya unga na mche, taulo za kile, nguo za ndani pamoja na tatulo za watoto.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Isanga Sehemu ya Wanawake, Mrakibu wa Magereza Sifa Anyimike ameipongeza TSC kwa kutoa msaada huo huku akieleza kuwa misaada inayotolewa na wadau mbalimbali inasaidia Serikali kupunguza gharama za uendeshaji wa magereza huku akifafanua kuwa misaada yote inayotolewa katika gereza hilo inawafikia walengwa na kutumika kwa lengo lililokusudiwa.

 

“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa TSC kwa kuwaletea misaada wanafunzi (wafungwa) wetu wa kike. Misaada hii itawasaidia sana kwa kuwa wana mahitaji mbalimbali. Misaada hii inatija sana kwetu kwa kuwa pamoja na kuwa inawasaidia wafungwa, inaleta pia ahueni kwa Serikali kwani inasaidia kupunguza gharama katika kuhudumia magereza,” amesema.  

 

Ameongeza, “Napenda niwatoe wasiwasi juu ya misaada inayotolewa kwenye gereza letu. Hii mizigo yote inawenda kwa wahusika kwa uwazi kabisa kwa sababu wanaoleta msaada wanaonana na wafungwa na lazima wawaambie ni msaada gani wameleta na wao (wafungwa) wana daftari lao, wanaandika kila kitu kinacholetwa na wanatumia vitu hivyo wenyewe.”

 

Mkuu huyo wa gereza ametoa wito kwa taasisi na jamii kwa ujumla kuendelea kujitokeza kutoa misaada kwenye gereza hilo huku akitaja vifaa vinavyohitajika sana kuwa ni masweta ya rangi ya kijani na bluu, sukari, sabuni, mfuta na blanketi.

 

Kauli mbiu ya maandimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2023 ni, “Kufanikiwa kwa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (Acfta) Kunahitaji Usimamizi wa Utumishi wa Umma wenye Mtazamo wa Kikanda”.