TSC YATOA MAFUNZO UTUMIAJI WA MFUMO WA TSCMIS

12 Oct, 2022
TSC YATOA MAFUNZO UTUMIAJI WA MFUMO WA TSCMIS

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeendesha mafunzo ya uelewa wa ufanyaji kazi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Tume (TSCMIS) ikiwa ni mwanzo wa matumizi ya mfumo huo unaolenga kurahisisha utoaji wa huduma katika masuala ya Ajira, Maadili na Maendeleo ya Walimu nchini.

Akifungua Mafunzo hayo yanayofanyika Oktoba 10 - 13, 2022 katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine kampasi ya Mazimbu – Morogoro, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama alisema kuwa mfumo wa TSCMIS utarahisisha na kuboresha utendaji kazi wa shughuli za kila siku katika kuwahudumia walimu kwenye masuala ya ajira (usajili na kuthibitishwa kazini), maendeleo ya Walimu (kupandishwa vyeo na kubadilishiwa muundo wa utumishi), mafao, mashauri ya nidhamu pamoja na rufaa za walimu.

“Matumizi ya mfumo yataongeza ufanisi katika kushughulikia Utumishi wa Walimu na utamfanya mwalimu asihangaike kutafuta huduma. Kama atakuwa na hoja zake ataingia kwenye mfumo atatoa taarifa ataweka na hoja yake atatuma. Akishatuma ana uwezo wa kufuatilia na kuona hoja yake ilipofikia na pale itakapokuwa imejibiwa atapata majibu hapo hapo. Hivyo, kwa kupitia simu ya mkononi mwalimu atapata huduma zote za kiutumishi,” alisema Nkwama.

Aliongeza kuwa mfumo huo utasaidia kuondoa changamoto za upatikanaji wa taarifa kwa wakati hususan taarifa za wilaya ambazo mara kwa mara zinachelewa kuwasilishwa TSC Makao Makuu kwa kuwa mfumo huo una uwezo wa kutunza na kutoa taarifa ya kila kinachofanyika kuanzia ngazi ya shule hadi TSC Makao Makuu.

Aidha, Katibu huyo aliongeza kuwa miongoni mwa majukumu ya TSC ni kushughulikia mashauri ya nidhamu ya walimu kwa haki na kueleza kuwa kutumika kwa mfumo huo kutasaidia Tume hiyo kutasaidia kuondoa changaoto mbalimbali katika kuendesha mashauri kwenye ngazi ya shule na ngazi ya wilaya.  

“Katika uendeshaji wa mashauri ya nidhamu kumekuwa na changamoto ndogondogo ambazo wakati mwingine zimesababisha mashauri ya walimu kuchalewa kumalizika. Pale unapokuta shauri limeendeshwa lakini taratibu zimekiukwa, mwalimu anapokata rufaa shauri hilo linarudishwa lianze upya. Lakini kupitia mfumo huu tutakuwa na uwezo wa kuona shauri tangu linapofunguliwa, hivyo kama tutaona kuna sehemu haiko sawa ni rahisi kutoa ushauri stahiki mapema,” alisema.

Nkwama alisisitiza kuwa mara baada ya mafunzo hayo anataka mfumo huo uanze kutumika huku akiweka bayana kuwa hatakubali kuona wilaya ambazo zimepata mafunzo zinaleta visingizio vya kutotumia mfumo huo na kuwataka washiriki hao kuwa mfano mzuri katika matumizi ya mfumo huo.

“Sasa ninyi ni mmekuwa mabalozi, ninatarajia kuwa baada ya kutoka hapa mtakwenda kuutumia mfumo huu kama inavyotakiwa. Tukumbuke wakuu wa shule wanasajili wanafunzi kwa ajili ya kufanya mitihani ya Taifa kwa mfumo. Sasa itakuwa ni jambo lisiloeleweka kwa wewe mtumishi wa TSC kuanza kuleta visingizio ili tu usitumie mfumo, kwa kweli hatutaelewana,” alisema Nkwama.

Nkwama pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwajali walimu na kuamua kuitengea TSC bajeti kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa mfumo huo. Vilevile, alitumia fursa hiyo kimpongeza Mhe. Angellah Kairuki kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambapo alieleza kuwa Waziri huyo ameelekeza kuongeza kasi ya matumizi ya mifumo ya kielektoniki katika shughuli za Serikali ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Awali akitoa taarifa za maendeleo ya mfumo huo, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa TSC ambaye pia ni Mratibu na Msimamizi wa ujenzi wa mfumo huo, Bi. Kainda Ndassa, alisema kuwa ujenzi wa mfumo huo uliochukua muda wa miaka miwili ulikamilika tarehe 31/08/2022 ambapo kwa nyakati tofauti ulihusisha wataalam kutoka Taasisi mbalimbali ikiwewo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ofisi ya Rais Menejeimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mamlaka ya Serikali Mtandao na Vyuo Vikuu vya Sokoine na Mzumbe.

“Ninawashukuru Maafisa Wataalamu wote wa TEHAMA kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), na Chuo Kikuu Mzumbe) kwa kuratibu zoezi zima la uundaji wa mfumo huu,” alisema.

Alisema kuwa ujenzi wa Mfumo wa TSCMIS ambao unajumuisha moduli sita (6) umezingatia Mwongozo uliotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) na kufuata hatua mbalimbali katika ujenzi wake ambazo ni pamoja na kubainisha mahitaji (Requirement gathering), kusanifu na kujenga Mfumo (System Design and Development), majaribio (Testing), kusimika na kusimamia Mfumo (Operational and Maintenance).

Alizitaja moduli hizo kuwa ni 'Disciplinary, Appeal, Gratuity and Pension Computation, Complaints, Registration, Visitors and Helpdesk' ambazo zinahusika na uendeshaji wa mashauri ya nidhamu na rufaa, ukokotoaji wa mafao ya ajira za mkataba, malalamiko na dawati la msaada kwa wateja.

Mafunzo hayo yaliwahusisha watumishi wa TSC kutoka Wilaya za Mikoa ya Mwanza, Iringa, Dodoma, Dar es Salaam na Wilaya ya Morogoro ambaye ni mwenyeji wa mafunzo hayo huku Wilaya ya Kishapu ikishariki kama Wilaya ya mfano. Vilevile baadhi ya Wakuu wa Shule kutoka Shule za Msingi na Sekondari walishiriki.