TSC YAWAJENGEA UWEZO WAJUMBE WA KAMATI YA UKAGUZI WA NDANI

13 Jun, 2023
TSC YAWAJENGEA UWEZO WAJUMBE WA KAMATI YA UKAGUZI WA NDANI

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeendesha mafunzo ya Kamati ya Ukaguzi wa Ndani ya TSC kwa lengo la kuwajengea uelewa wajumbe wa kamati hiyo, Menejimenti na Maafisa Bajeti wa Tume juu ya masuala ya ukaguzi, mfumo wa ufuatiliaji  na utekelezaji wa  mapendekezo ya Hoja za  Ukaguzi na vihatarishi ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo.

 

Akifungua mafunzo hayo tarehe 12 Juni, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kiwete jijini Dodoma, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama amesema TSC imeona kuna haja ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi pamoja na watumishi wengine wa Tume hiyo ili kuongeza uelewa katika kutekeleza majukumu yao.

 

Natambua umuhimu wa Kamati hii kupatiwa mafunzo, kwani ipo kwa Mujibu wa sheria ya fedha za umma sura 348, Kanuni ya 30 ya Kanuni za Fedha za mwaka 2001. Aidha, Kamati ya Ukaguzi wa ndani ina jukumu la kuhakikisha kuwa shughuli za ndani za Taasisi zinafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria na kanuni na katika kutekeleza hilo Majukumu ya  Kamati  yameelezwa katika Kanuni ya 32 (1) (a) – (g),” amesema Nkwama.

 

Katibu huyo ameeleza kuwa ushauri unaotolewa na Kamati hiyo umekuwa ukifanyiwa kazi na jambo ambalo limesaidia TSC kupata mafanikio mbalimbali.

Miongoni mwa mafanikio aliyoyataja ni kupata Hati safi; kuendelea kuimarishwa kwa Sehemu ya Ukaguzi kabla ya malipo (Pre Audit Section); Kuandaliwa kwa Mwongozo wa Usimamizi wa Vihatarishi (Risk Management Framewok)  kulingana na Mpango Mkakati wa Taasisi 2021/22 hadi 2025/26 ambao uliwezesha kuandaliwa kwa Daftari la Vihatarishi la Taasisi (Risk Register); na Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kuongezewa mtumishi.

 

“Tukipokea na kufanyia kazi ushauri unaotolewa na Kamati katika masuala ya Ukaguzi wa Ndani, Ukaguzi wa Nje, Taarifa za Fedha, Usimamizi wa Viashiria hatarishi, Mifumo ya Uthibiti wa Ndani na Uendeshaji wa jumla wa shughuli za Taasisi (Tume) kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu. Kwa wakati wote, lengo la ushauri limekuwa ni  kuongeza ufanisi na tija kwa Tume,” amesema Mwl. Nkwama.

 

Sambamba na hilo, Mwl. Nkwama amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na jitihada zake za kuboresha Sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kutafuta wadau  wa maendeleo ili kuendeleza miradi ya elimu, kuajiri na kupandisha madaraja walimu, kujenga nyumba za walimu na kuendelea kujenga miundombinu ya shule.

 

 

Sote tumeshuhudia ujenzi wa madarasa kuanzia elimu ya awali, Msingi na Sekondari nchi nzima. Kupitia Sera ya Elimu bila malipo Serikali imeweza kujenga madarasa 3,000 kwa Shule za Msingi. Kupitia Mradi wa SEQUIP ambao umelenga kuboresha elimu ya Sekondari, Serikali imepanga kujenga Shule za Sekondari 1,026. Kati ya shule hizo 282 zimejengwa ngazi ya Kata, Shule 26 za bweni kwa wasichana zinajengwa huku jumla ya shule 184 ikiwa ni shule moja katika kila Halmashauri zimeidhinishwa zijengwe, huku shule 10 kati ya hizo zikielekea kwenye ukamilifu,” amesema.

 

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Upendo Werema ambaye ni mtumishi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango amesema mafunzo hayo yataisaidia wajumbe wa Kamati kuzielewa kwa kina Sheria na taratibu za Nchi na za Kimataifa zinazohusiana na masuala ya ukaguzi na hivyo kuzizingatia katika kutekeleza majukumu yao.

 

Ameongeza kuwa Kamati hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kutoa ushauri stahiki utakaoiwezesha TSC kuzingatia taratibu ili kuepuka kupata hoja za ukaguzi.

 

Kwa Upande wa Katibu wa Kamati hiyo, Laurence Chankan amesema mbali na wajumbe wa kamati ya ukaguzi mafunzo hayo yameshirikisha Sekretarieti ya Kamati ya Ukaguzi, Wawakilishi wa Menejimenti ya Tume ambao, Mratibu wa vihatarishi pamoja na Maafisa Bajeti wa Idara na Vitengo  ambao pia ni risk champions wa maeneo wanayoyawakilisha.

 

“Ushirikishwaji huu unalenga kuwa na ueleewa wa pamoja katika kutekeleza majukumu ya Kamati na Tume kwa ujumla wake. Katika mafunzo haya mambo yatakayo fundishwa ni pamoja na-; Effective internal auditing  in Public Sector, Internal Audit Processes, Internal Audit Charter, Introduction to Audit Committee  Guideline, Roles & Responsibilities of Audit Committee, Meetings & Conduct of Audit Committee, Relationship of Audit Committee  with Key Stakeholders, Performance Evaluation of Audit Committee na Elements of Audit Committee Charter” amesema Chankan.

 

Aliongeza kuwa mafunzo hayo pia yatahusisha masuala ya vihatarishi na kuhusu  mfumo mpya wa ufuatiliaji  na utekelezaji wa  mapendekezo ya Hoja za  Ukaguzi  kwa  wakala wa serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma  ambapo mfumo huo utasaidia Taasisi kuwasilisha taarifa za ukaguzi za kila robo mwaka na taarifa za mwaka  kwa wakati.

 

Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 12 hadi 15 juni 2023 na mwezeshaji mkuu ni Bw. Alfonce Muro kutoka Ofisi ya mkaguzi Mkuu wa Ndani.