TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA YAITEMBELEA TSC KUPATA UZOEFU WA UTENDAJI KAZI

03 Nov, 2024
TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA YAITEMBELEA TSC KUPATA UZOEFU WA UTENDAJI KAZI

Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bibi Alesia Mbuya ametembelea Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwa lengo la kujifunza namna TSC inavyotekeleza majukumu yake katika kusimamia Walimu.

 

Naibu Katibu huyo aliyeambatana na afisa kutoka Tume hiyo, Bibi Salome Stephano ametembelea TSC tarehe 1 Oktoba, 2024 na kupokelewa na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina Nkwama ambapo pamoja na mambo mengine Bibi Alesia alipata fursa ya kukutana na Kamati Maalum ya TSC inayohusika na kuchambua rufaa za walimu.

 

Bibi Alesia alisema kuwa lengo la kufanya ziara hiyo ni kujifunza namna ambavyo TSC inatekeleza majukumu yake ikiwa ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu kwa kuwa majukumu yake yanaendana na yale ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa Watumishi wa Mahakama.

 

Alieleza kuwa kuna maeneo makuu matatu ambayo Tume ya Utumishi wa Mahakama inapenda kuyafahamu kwa kina ambayo ni Muundo wa Tume ya Utumishi wa Walimu, namna mashauri ya nidhamu yanavyoendeshwa na Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Sura 448 kwa ujumla wake.

 

Kwa upande wa Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama alisema kuwa pamoja na kwamba TSC na Tume ya Mahakama kila moja inatekeleza sheria yake, Taasisi hizo pia kuna wakati hulazimika kutumia Sheria ya Tume ya Utumishi wa Umma Sura 298 ambayo ndiyo Sheria mama katika kusimamia Utumishi wa Umma.

 

“Ni muhimu sana kwa Tume ya Utumishi wa Walimu na Tume ya Utumishi wa Mahakama kukutana na kupeana uzoefu kwa kuwa tunatekeleza majukumu yanayoendana. Kubadilishana uzoefu kunatoa fursa ya kila upande kujifunza kutoka kwa mwenzake kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa wetu,” alisema Mwl. Nkwama.

 

Katika Kikao hicho TSC iliwasilisha mada juu ya Muundo na Majukumu ya Tume ya Utumishi wa Walimu, Taratibu za Uendeshaji wa Vikao vya Tume na Kamati za Tume za Wilaya, Mchakato wa Nidhamu kwa Walimu pamoja na Mchakato wa Rufaa.