UJENZI OFISI ZA TSC MAKAO MAKUU WAFIKIA ASILIMIA 18

16 Jun, 2023
UJENZI OFISI ZA TSC MAKAO MAKUU WAFIKIA ASILIMIA 18

Kamati ya Ukaguzi ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), tarehe 16 Juni 2023 imetembelea mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya TSC Makao Makuu unaotekelezwa katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma na kuelezwa kuwa utekelezaji wake umefikia asilimia 18.

Wajumbe wa Kamati hiyo walioongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati, Upendo Werema wamefanya ziara hiyo kwa lengo la kuangalia hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi pamoja na kufuatilia kuona kama mapendekezo yaliyotolewa na Kamati kwenye mradi huo yamefanyiwa kazi.

 

Akitoa maelezo juu ya hatua iliyofikiwa, Mhandisi wa ujenzi wa mradi huo kutoka Shirika la SUMAJKT, Sarah Sekwao amesema kazi inayoendelea ni kusambaza na kushindilia mawe na kisha kumwaga zege huku akieleza kuwa ujenzi huo umefikia asilimia 18 ikiwa ni asilimia mbili nyuma ya mpango kazi ambapo ujenzi huo ulitakiwa uwe umifikia asilimia 20.

 

“Awali, wakati tupo kwenye hatua ya uchimbaji wa mashimo ya nguzo tulikukutana na miamba migumu tofauti na tulivyokuwa tumetarajia. Hivyo, ilitulazimu kutafuta vifaa vya ziada kwa ajili ya kuchimba na kupasua miamba. Hili lilisababisha kuchelewa kwa hatua za utekelezaji wa mradi ikilinganishwa na mpango kazi,” akisema Mhandisi Sarah.

 

Hata hivyo, ameeleza kuwa badada kutokea kwa changamoto zilizosababisha utekelezaji wa mradi kuwa nyuma walizingatia maelekezo ya Kamati hiyo iliyowataka kupitia upya mpango kazi wao na kufanya marekebisho ili kuhakikisha uradi huo hauchukui muda mrefu kukamilika tofauti na mkataba.

 

“Tuna imani kuwa mradi huu utakamilika kwa wakati. Huko chini ndio kulikuwa kugumu kutokana na changamoto tulizokutana nazo, lakini kwa huku juu hakuna changamoto, hivyo kasi ya utekelezaji itaongezeka na katika muda mfupi ujao tutakwenda sambamba na mpango kazi,” amesema Mhandisi huyo.

 

Kamati hiyo pia ilitaka kujua ubora wa jengo hilo ambapo Mhandisi Sarah alieleza kuwa kwa kila hatua wamekuwa wakizingatia vigezo vyote na kufanya kile kinachotakiwa hivyo jengo hilo litakamilika likiwa katika ubora uliopangwa.

 

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Upendo Werema amesema Kamati hiyo imeridhishwa na namna kazi inavyoendelea kufanyika huku akisisitiza kuwa ni muhimu kuongeza kasi zaidi ya utekelezaji ili mradi ukamilike kwa wakati.

 

Vilevie, Werema aliagiza kupata nakala ya marekebisho ya mpango kazi ili kuiwezesha Kamati ya Ukaguzi kuona kama marekebisho hayo yatawezesha mradi huo kukamilika kwa muda uliopangwa.