HEKO SERIKALI KWA JITIHADA MADHUBUTI ZA KUBADILISHA MUUNDO WA UTUMISHI WA WALIMU NCHINI NA UWEZESHAJI WA WARSHA ELEKEZI KWA WALIMU WA AJIRA MPYA NDANI YA SIKU 365 ZA MAMA SAMIA – TSC BARIADI

08 Apr, 2022
HEKO SERIKALI KWA JITIHADA MADHUBUTI ZA KUBADILISHA MUUNDO WA UTUMISHI WA WALIMU NCHINI NA UWEZESHAJI WA WARSHA ELEKEZI KWA WALIMU WA AJIRA MPYA NDANI YA SIKU 365 ZA MAMA SAMIA – TSC BARIADI

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, imeadhimisha mwaka mmoja wa utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kupongeza na kuunga mkono jitihada madhubuti za Serikali kupitia TSC Makao Makuu za kubadilisha Muundo wa Utumishi wa Walimu nchini, kuridhia kubadilishwa kwa Muundo wa TSC, upandishaji walimu madaraja baada ya baadhi yao kukaa miaka mitano hadi sita bila kupandishwa huku wakiwa na sifa za kupanda tangu mwaka 2016 pamoja na uwezeshaji wa warsha elekezi kwa walimu wa ajira mpya zilizotolewa katika kipindi hicho.

Akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kutoka Ofisi za Tume Makao Makuu, Ndg. Gerard Chami, hivi karibuni akiwa ziarani katika mikoa ya Simiyu na Mara, Kaimu Katibu Msaidizi (KKM) wa TSC Bariadi, Ndg. Wang’eng’I Mohabe, alisema; Serikali imefanya kazi kubwa ya utekelezaji wa ahadi na mahitaji muhimu ya walimu ambayo yameongeza tija katika utoaji taaluma kwa wanafunzi ikiwemo ubadilishwaji wa muundo wa utumishi wa walimu na upandishaji walimu madaraja uliositishwa kwa takribani miaka sita iliyopita tangu 2016 jambo lililorudhisha sana nyuma bidii ya walimu katika usimamizi na utoaji huduma hiyo.

KKM Mohabe alisema; “Kwakweli tunajivunia uongozi, utendaji, na utekelezaji wa ahadi za msingi wa Mama Samia kwa walimu wetu tunaowasimamia ambao ndiyo umeleta maarifa zaidi, ari, tija na morali ya uwajibikaji mahali pa kazi, ushirikiano mzuri baina yao na wanafunzi, kupungua kwa kiasi kikubwa kwa malalamiko ya walimu katika nyanja mbalimbali hasa muundo na madaraja, uvumilivu na usikivu katika utumishi wa umma ambao kwasasa unaufanya mkoa wetu wa Simiyu kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vema kitaaluma.”

Pamoja na hilo KKM Mohabe alisema TSC Wilaya ya Bariadi inayohudumia Halmashauri mbili yaani Bariadi Mji na Bariadi Wilaya haina shule shikizi hata moja baada ya zote kukamilisha na kupata usajili na hivyo wanahudumia jumla ya shule 169 zikiwa 59 (Msingi 43 na 16 Sekondari) ziko Halmashauri ya Mji wa Bariadi na 110 (Msingi 86 na 24 Sekondari) ziko Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.

Wakati huohuo KKM Mohabe akiwekea mkazo mwendelezo wa utoaji elimu kwa umma na wateja wanaohudumiwa na ofisi zote za TSC nchini, aliiomba Ofisi ya TSC Makao Makuu kutengeneza na kusambaza katika ofisi zote za wilaya zana za uelimishaji yakiwemo mabango ya kusimamisha, vipeperushi na vijarida ili kutumika kama vielelezo nyakati zote za utoaji elimu kwa umma, wateja na wadau wote muhimu juu ya kazi na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Walimu kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha TSC.

Vilevile, Afisa Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC Wilaya ya Bariadi, Ndg. Abraham Maiga, akielezea eneo ambalo wanajivunia katika seksheni ya ajira na maendeleo ya walimu alisema, sehemu kubwa ya walimu wanaohudumiwa na ofisi yao wameweza kujiendeleza kitaaluma kwa ngazi mbalimbali baada ya mwajiri kuridhia kwenda mafunzoni kwa walimu katika nyakati tofauti yakiwemo mafunzo ya muda mrefu na mfupi hivyo kuwa na weledi wa kutosha katika kufuata Sheria, Kanuni, na Taratibu za kazi huku uwajibikaji katika kufundisha ukiongezeka.

Nae Afisa Nidhamu na Maadili ya Walimu kutoka TSC Wilaya ya Bariadi, Ndg. Ramadhani Irunde, akitaja baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo kama ofisi na wanazokabiliana nazo walimu alisema ni pamoja na baadhi ya walimu kuingia katika madeni makubwa yanayopelekea baadhi yao kuwa watoro kazini na wakati mwingine kuacha kazi kabisa, kutokubalika kwa baadhi ya barua za walimu za kupanda madaraja katika mfumo wa mshahara hivyo kukatisha tamaa na kupunguza ufanisi kazini.

Ofisi ya TSC Bariadi inahudumia jumla ya Halmashauri mbili; Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi zikiwa na jumla ya walimu 2,363 (Halmashauri ya Mji wa Bariadi ikiwa na jumla ya Walimu 995; Msingi walimu 729 ambapo Wanawake ni 400 na 329 ni Wanaume na Sekondari walimu 266 ambapo Wanawake ni 80 na 186 ni Wanaume huku Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ikiwa na jumla ya walimu 1,368; Msingi walimu 1,061 ambapo Wanawake ni 316 na 745 ni Wanaume na Sekondari walimu 307 ambapo Wanawake ni 65 na 242 ni Wanaume).