VIONGOZI TSC WATEMBELEA ENEO LA KIWANJA CHA TUME HIYO NJEDENGWA, DODOMA

10 Jun, 2022
VIONGOZI TSC WATEMBELEA ENEO LA KIWANJA CHA TUME HIYO NJEDENGWA, DODOMA

Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wakiongozwa na Mwenyekiti na Katibu wa Tume hiyo wametembelea kiwanja cha TSC kilichopo eneo la Njedengwa jijini Dodoma ambapo maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa ofisi za Tume Makao Makuu yanendelea kufanyika.

Viongozi hao walifanya ziara hiyo Mei 25, 2022 kwa lengo la kufahamu eneo hilo na kujionea hatua iliyofikiwa katika hatua za awali za maandalizi ya kuanza kwa ujenzi huo ambapo walimkuta mkandarasi akiendelea na kazi ya kusafisha eneo huku baadhi ya vifaa vya kazi vikiwa vimefikishwa kwenye eneo hilo.

Akiwa katika eneo hilo, Mwenyekiti wa TSC, Prof. Willy Komba alimweleza Mkandarasi kutoka SUMA JKT ambao ndio wanaojenga jengo hilo kuwa TSC inatarajia kuwa ujenzi huo utakwenda kwa kasi ili ukamilike katika kipindi kilichopangwa.

“Mimi na Makamishna wenzangu tumeteuliwa kushika nafasi hizi kwa kipindi cha miaka mitatu, na tunatamani tuone ofisi za Tume zinajengwa kabla muda wetu haujamalizika. Hivyo, nikuombe Mkandarasi hakikisheni ujenzi huu unakwenda kwa kasi kwa kuwa malipo ya awali tayari tumeshawalipa, hakuna sababu inayofanya ujanzi huu usiende kwa wakati,” alisema.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa ameridhishwa kuona kuwa shughuli za kusafisha kiwanja zimeanza na baadhi ya vifaa tayari vimewasili kwenye eneo hilo, hivyo anatarajia kuwa kazi ya rasmi ya ujenzi itaanza katika kipindi cha muda mfupi.

“Ninashukuru kuona kuwa angalau sasa kuna dalili kwamba muda si mrefu ujenzi rami wa jengo utaanza. Ninaona tayari mmesafisha uwanja na mmeanza kuleta vifaa, ninachowaomba pamoja na kwamba huenda mna kazi nyingi za ujenzi hakikisheni ujenzi huu manaupatia kipaumbele ili walimu waweze kuhudumia katika mazingira bora,” alisema Prof. Komba.

Kwa upande wake Katibu wa TSC, Paulina Nkwama alisema kuwa TSC itaendelea kufuatilia kwa karibu ujenzi huo na kuhakikisha kwamba kazi hiyo inafanyika kwa kasi na kwa ubora ili serikali iweze kufikia malengo yake katika kutoa huduma kwa walimu.

Aliongeza kuwa, katika bajeti ya 2021/2022 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni mia tano (500,000,000) kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi huo ambapo zaidi ya shilingi 360, 000, 0000 zimeshalipwa kwa SUMA JKT kwa ajili ya kuanza shughuli za ujenzi huo.

“Kuanzia sasa ziara za kuja hapa hazitakoma, tutakuja mara kwa mara ili kuona namna ujenzi huu unavyokwenda. Tunamshukuru pia Rais wetu, Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za kuanza kwa ujenzi huu na ni imani yetu kuwa ataendelea kutupatia fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huu,” alisema Katibu huyo. 

Naye Mkandarasi kutoka SUMA JKT amewahakikishia viongozi hao wa TSC kuwa kazi hiyo itafanyika kwa kasi ili kuendana na muda uliowekwa huku akisisitiza kuwa watawashirikisha TSC kwa kila hatua ya ujenzi ili kuhakikisha jengo linalojengwa linakidhi matarajio.