WAJUMBE TENGENI MUDA KUTEMBELEA OFISI ZA TSC ZILIZOPO KATIKA MAENEO YENU: PROF MURUKE
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Masoud Muruke ametoa wito kwa Wajumbe wa TSC kutembelea ofisi za Tume hiyo ngazi ya Wilaya zilizopo karibu na maeneo yao kwa lengo la kupata maoni na kufahamu changamoto zinazowakabili watumishi katika maeneo hayo.
Prof. Muruke ametoa kauli hiyo tarehe 28 Agosti, 2024 wakati akiendesha Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Walimu unaofanyika mjini Morogoro.
Alisema kuwa Wajumbe wa Tume wana wajibu wa kusimamia na kuhakikisha Ofisi zote za TSC zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika kutoa huduma kwa walimu.
“Mimi mwenyewe jana niliona ni vema kutembelea Ofisi za Tume Wilaya ya Morogoro kwa kuwa nipo hapa Morogoro. Tukitembelea ofisi zetu hizi tunapata fursa ya kufahamu mazingira ya kazi ambayo wenzetu wanafanyia kazi. Pia, inasaidia kupata maoni yao na kufahamu changamoto zinazoweza kukwamisha utoaji wa huduma bora kwa walimu,” alisema.
Aliongeza kwa kusema kuwa, “kwa kutembelea ofisi zetu, inatusaidia kuwa katika mazingira mazuri ya kufanya maamuzi sahihi kwa maslahi ya maendeleo ya walimu.”
Prof. Muruke aliwaeleza Wajumbe hao kuwa wanaweza kutembelea ofisi hizo bila kutumia gharama kubwa hususan kwa ofisi zilizo karibu na maeneo yao au pale wanapokuwa na ziara binafsi au za kazi kupitia ofisi wanazofanyia kazi.