WALIMU 258,291 NA WADAU WENGINE KUNUFAIKA NA TOVUTI MPYA YA TUME BAADA YA WADAU WA AWALI 182,650 KUNUFAIKA NA ILE YA AWALI

27 May, 2022
WALIMU 258,291 NA WADAU WENGINE KUNUFAIKA NA TOVUTI MPYA YA TUME BAADA YA WADAU WA AWALI 182,650 KUNUFAIKA NA ILE YA AWALI

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Lazaro Komba, leo katika Mkutano wa Tume amezindua tovuti mpya ya TSC inayotarajiwa kuhudumia Walimu wapatao 258,291 ambao ni Walimu 173,591 wa Shule za Msingi na Walimu 84,700 wa Sekondari tofauti na Wadau mbalimbali 182,650 walionufaika na tovuti ya awali iliyokua na changamoto kadhaa. 

Akiongea na washiriki wa hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika Jijini Dodona katika Ukumbi wa Chama cha Mapinduzi (Jakaya Kikwete Convention Center) alisema pamoja na kuhudumia walimu, hao tovuti mpya itawahudumia pia wadau wengine wote wa Sekta ya Elimu, Taasisi, Wananchi na Taifa kwa ujumla. 

Prof.Komba alisema, “Kwa kipindi cha miaka saba sasa (2017 - 2022) tangu Tume kuwa na tovuti, taarifa na mambo mbalimbali ya TSC ambayo Tume ingependa yawafikie walengwa na jamii kwa ujumla kwa wakati tarajiwa ili kufikia malengo ya utekelezaji zimekua haziwafikii kama ilivyotarajiwa kutokana na changamoto za hapa na pale zilizobainishwa ikiwemo changamoto ya mabadiliko makubwa ya kiteknolojia duniani katika eneo la Habari, Elimu, Mawasiliano na Uhamasishaji. 

Aidha, kabla ya kuzindua tovuti hiyo; aliwaelekeza na kuwasisitiza Maafisa TEHAMA na Mawasiliano ya Serikali katika uendeshaji wa tovuti pamoja na zana nyingine zote za mawasiliano na jamii, uhabarishaji, uelimishaji na uhamasishaji ikiwemo mitandao ya jamii, kuzingatia viwango, maelekezo na miongozo yote ya Serikali kwani pamoja na kufuata maelekezo hayo wamewezeshwa kwa mafunzo kuwa na umiliki wa moja kwa moja wa zana hizo za mawasiliano hali inayosababisha uhuishaji wa taarifa na kufanya maboresho mbalimbali kwa wakati kuwa rahisi. 

Hali kadhalika, Prof. Komba alisema kuwa ni matumaini yake kuanzia sasa taarifa zote hai zenye tija kwa Walimu, Wateja, Wadau na Jamii kwa ujumla wake zitapatikana kwa wakati zikiwa hai na zenye tija kwa walengwa ikiwa ni pamoja na kuwezesha wateja kupata huduma muhimu za Tume kupitia tovuti hiyo mpya bila kulazimika kutembelea Ofisi za Tume Makao Makuu au katika Ofisi za Tume ngazi ya Wilaya zote 139. 

“Imeelezwa hapa kuwa tovuti mpya iliyoboreshwa itakuwa chanzo sahihi na bora kwa Walimu, Wateja na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Elimu kupata taarifa mbalimbali za Tume. Ni wazi taarifa na maudhui yatakayowekwa kwenye tovuti yatatumika kwa usahihi katika kazi mbalimbali ikiwemo kujifunza, kufanya tafiti, kupata huduma na rejea ya nyaraka mbalimbali kuhusu masuala ya Utumishi wa Walimu. Nawasihi wadau wote hususan walimu kuitumia tovuti hii kupata huduma, taarifa, maudhui, takwimu na nyaraka mbalimbali kwa rejea na matumizi sahihi.” Alisema Mwenyekiti huyo wa TSC 

Aliwashukuru wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha zoezi la kutengeneza tovuti hiyo iliyogharimu Tzs.6,000,000/= wakiwemo Wadau wa Maendeleo ambao alisema ndiyo msaada na chanzo cha awali cha kuifanikisha Tume kuwa na tovuti, na kipekee aliwashukuru sana Makamishna wa Tume kwa ushirikiano wao, Wajumbe wa Menejimenti ya TSC kwa utekelezaji kwa wakati, vilevile Kamati ya TEHAMA ya Tume kwa maoni na ushauri wao, na Idara na Vitengo vyote kwa kuwezesha mchakato wa kumpata mzabuni wa kutekeleza kazi hiyo ikiwa ni pamoja na kuandaa maudhui na taarifa mbalimbali ambazo zitatumika kwenye tovuti hii. 

Kwa namna ya pekee Prof. Komba alivipongeza Kitengo cha TEHAMA na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali vya Tume kwa uratibu wa zoezi zima la matengenezo ya tovuti hiyo kwa pamoja na Watalaam wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,

Wizara ya Fedha na Mipango (MoFP) na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa ushauri na kazi kubwa ya kutengeneza tovuti na kuwapa mafunzo Maafisa Watalaam wa Tume. 

Nae Katibu wa Tume, Mwl. Paulina Nkwama, kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Tume, Prof. Willy Komba, alizitaja baadhi ya changamoto zilizopelekea maelekezo ya Tume kwa Menejimenti ya Tume kutengenezeza tovuti mpya kuwa ni pamoja na; tovuti ya awali kutengenezwa kwa teknolojia ya zamani, waendeshaji tovuti kutokuwa na uelewa wa kutosha kwenye masuala ya usimamizi wa tovuti hiyo, uhitaji mkubwa wa kuboresha mwonekano  na maudhui  ya tovuti, uelewa hafifu na usio fasaha wa namna ya kuandaa na kupandisha taarifa, takwimu na nyaraka mbalimbali kwenye tovuti, Maafisa TEHAMA, Habari na Mawasiliano kutokuwa na umiliki wa moja kwa moja (ownership) hali ambayo ilisababisha changamoto katika kuhuisha taarifa na kufanya maboresho mbalimbali kwa wakati, na tovuti kutokidhi mahitaji ya Tume kwa kutokuwa na maeneo ya kutosha kwa ajili ya kuweka taarifa mbalimbali za

Taasisi. 

Katibu huyo alisema, “Tofauti na tovuti ya awali, tovuti hii mpya ni bora zaidi kwa kuwa; inakidhi mahitaji ya Tume kutokana na uwezo wake wa kubeba taarifa nyingi zaidi kwa wakati mmoja, inaendana na teknolojia ya kisasa, ina uwezo mkubwa wa kuingiza na kupokea maudhui na maboresho ya taarifa kwa wakati, Maafisa wa TSC (TEHAMA na Mawasiliano ya Serikali) kupitia mafunzo yaliyotolewa wana uelewa wa kutosha katika usimamizi (administration) na uendeshaji, na tovuti hii inamsaidia mtumiaji (Walimu na wadau wengine wa Tume) kupata viunganishi (links) vya mifumo mingine mbalimbali kwa urahisi.” 

Akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa tovuti ya Tume kabla ya uzinduzi Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa Tume, Gerard Chami, alisema pamoja na faida zilizoainishwa huduma na vitu vitakavyopatikana katika tovuti hiyo mpya ni pamoja na; Ufahamu wa Majukumu ya Tume kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha Tume, Sheria ya Tume na Kanuni zake, maelezo na taratibu za upatikanaji wa huduma mbalimbali zitolewazo na Tume, machapisho mbalimbali ikiwemo Miongozo, Mipango Mkakati, Tafiti, Taarifa, Sera, Majarida, Takwimu, Fomu mbalimbali za mtandaoni katika Utumishi wa Umma, na eneo la habari ambamo kutakua na Taarifa mbalimbali kwa Vyombo vya Habari, Hotuba, Vipeperushi, Vibango, Vibonzo, habari picha mnato, habari picha jongefu, Mawasiliano ya Tume pamoja na ramani mtandao ya kufika Ofisi za Tume Makao Makuu, Dodoma na Ofisi za Wilayani zote 139. 

Chami alisema vile tovuti mpya iliyoboreshwa itakuwa ni chanzo sahihi na bora cha taarifa mbalimbali kuhusu Tume kwa Walimu, Wananchi, Wadau wa Elimu na Taasisi mbalimbali, Kitengo cha TEHAMA kimejipanga vema kusimamia kikamilifu tovuti hiyo ili iweze kufanya kazi na kupatikana kwa muda wote huku Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali nacho kikiahidi kuhuisha taarifa kwa wakati na kwa kadri zinavyohitajika kwa walaji ili wadau wote waweze kupata taarifa kwa wakati na waweze kutumia huduma zilizopo kwenye tovuti hiyo. 

Kamishna Assela Luena akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa Tume, Kamishna Bahati Mgongolwa, alisema kukamilika kwa tovuti mpya ni jambo la kheri, lenye tija na manufaa makubwa kwa Tume na Taifa kwa ujumla wake kwani inaenda kuhudumia sehemu kubwa zaidi ya wateja wa TSC hususan Walimu, Wadau wa Elimu, Watafiti, Taasisi mbalimbali za Umma na Binafsi pamoja na Wananchi kwa ujumla na kupunguza uhaba wa awali wa upatikanaji wa taarifa mbalimbali muhimu kwa wateja wa Tume. 

Hafla hiyo ya uzinduzi wa tovuti mpya ya Tume ulihudhuriwa na Waheshimiwa Makamishna wa Tume, Katibu wa Tume, Wajumbe wa Menejimenti ya Tume, Wajumbe wa Kamati ya TEHAMA ya Tume, Mtaalamu mwakilishi kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Sekretarieti ya Mkutano wa Tume, Wanahabari na Watumishi wa Tume.