WALIMU 291 WILAYANI LONGIDO WAPATIWA ELIMU JUU YA UFAFANUZI WA KANUNI ZA MAADILI NA UTENDAJI KAZI KATIKA UTUMISHI WA WALIMU
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya ya Longido imefanikiwa kuzifikia shule 21 za msingi na sekondari na kutoa elimu kwa walimu 291 kuhusu ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji kazi katika Utumishi wa Walimu kwa lengo kusaidia walimu wilayani hapo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu.
Hayo yamebainika katika taarifa ya Kaimu Katibu Msaidizi wa TSC Wilaya ya Longido, Mwl. Tumaini Chugala iliyowasilishwa na Afisa wa TSC wa wilaya hiyo, Mwl. Boniphace Bita wakati wa ziara ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kutoka TSC Makao Makuu, Gerard Chami iliyolenga kupata taarifa juu ya utekelezaji wa majukumu ya Tume katika wilaya hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kabla ya kweda kutoa elimu kwa walimu, Kamati ya TSC Wilaya ya Longido ilifanya kikazo kazi cha kupitia ufafanuzi huo kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja na kisha wajumbe wa Kamati hiyo wakaamua njia madhubuti ya kufikisha elimu hiyo kwa walimu.
“Baada ya kupewa mafunzo na maelekezo kutoka TSC Makao Makuu ya kutoa elimu hii kwa walimu, sisi tulianza kutoa elimu kwa Wajumbe wa Kamati ambapo tulifanya kikao tarehe 14/03/2023. Baada ya hapo, Wajumbe hao walikubaliana kutafuta namna ya kufikisha elimu hiyo kwa walimu ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti, 2023 tumefanikiwa kuzifikia shule 21,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Shule za Msingi zilizofikiwa katika utoaji wa elimu hiyo ni; Longido, Oltepes, Elerai, Irkaswa, Tingatinga, Orbomba, Kimokoua, Engarenaibor, Buguruni, Matale, Kitarini, Sokon, Lopolosek, Losirwa, Endirma na Gelairumbwa.
Kwa upande wa shule za Sekondari zilizofikiwa ni; Lekule, Matale, Namanga na Enduimet.
TSC Wilaya ya Longido kwa kushirikiana na wadau wengine ambao ni Ofisi ya Mkurugenzi, Chama cha Walimu na Ofisi ya Mthibiti Ubora wa Shule katika Wilaya hiyo inafanya juhudi kuhakikisha walimu wote wanafikiwa na kupatiwa elimu hiyo muhimu.
Tume ya Utumishi wa Walimu Wilaya ya Longido inahudumia shule 63 ambapo kati ya hizo 54 ni za msingi na tisa (9) ni za Sekondari. Shule hizo zina jula ya walimu 735, kati ya hao 460 ni wa shule za Msingi na 275 ni wa shule za Sekondari.