WALIMU AJIRA MPYA WATAKIWA KUSOMA MIKATABA YA AJIRA NA KUTUNZA NYARAKA ZAO ZA KIUTUMISHI

16 Jun, 2023
WALIMU AJIRA MPYA WATAKIWA KUSOMA MIKATABA YA AJIRA NA KUTUNZA NYARAKA ZAO ZA KIUTUMISHI

Walimu 13,130 walioajiriwa hivi karibuni wametakiwa kusoma na kuielewa mikataba ya ajira zao kabla ya kuisaini na kuhakikisha wanatunza nyaraka zao za kiutumishi kwa ajili ya kumbukumbu na kurahisisha upatikanaje wake pale zinapohitajika.

Agizo hilo limetolewa tarehe 15 Juni, 2023 na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama wakati akifunga mafunzo ya Kamati ya Ukaguzi wa Ndani ya TSC yaliyowahusisha wajumbe wa kamati hiyo, Menejimenti na Maafisa Bajeti wa Tume hiyo  yaliyofanyika kwa siku nne katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Nkwama amesema, baadhi ya walimu wamejikuta wakitenda mambo mbalimbali kinyume na taratibu za kiutumishi kwa kukosa uelewa wa masharti ya mkataba wa ajira unaotokana na kutokusoma na kuielewa mikataba hiyo hivyo, kujikuta wakiingia kwenye matatizo kwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

“Ninaomba nitumie hadhira hii kuwakaribisha walimu wa ajira mpya 13,130 waliopangwa katika vituo mbalimbali vya kazi nchini. Tume ya Utumishi wa Walimu ipo tayari kutoa huduma na naamini maeneo ambayo wamepangwa wamekutana na makatibu Wasaidizi wa TSC katika kila wilaya kwa ajili ya kuwaongoza na kuwajazisha mikataba ya Ajira,” amesema Nkwama.

Kutokana na umuhimu huo wa kusoma nyaraka hizo, Nkwama amewaagiza Kaimu Makatibu Wasaidizi wa TSC katika Wilaya zote kuhakikisha wanapata muda wa kutosha wa kuwaelimisha walimu wapya kazini kuhusu mikataba hiyo na taratibu nyingine za kiutumishi kabla hawajaanza kutekeleza majukumu yao shuleni.

Sambamba na hilo, Nkwama amesema pamoja na kuwa Serikali ina utaratibu wa kutunza kumbukumbu za waajiriwa wake, bado mtumishi husika ndiye wa kwanza kuwajibika katika kutunza nyaraka zake.

“Nitoe rai, Mikataba hii ya ajira ambayo walimu wanaijaza, kwanza waisome kikamilifu, lakini pili nakala ya mkataba itunzwe. Custodian (mtunzaji) wa kwanza wa nyaraka za mwajiriwa ni mwajiriwa mwenyewe na wa pili ni kule alipoajiriwa.”

“Ninatambua kuwa ipo mifumo kama Human Capital Management Information System (HCMIS) ambayo inatunza taarifa za kiutumishi lakini hiyo haiondoi wajibu wa mtumishi mwenyewe kuhakikisha anakuwa na jalada lake ambalo ataweka nyaraka zake muhimu za kiutumishi au kuzihifadhi kwenye mifumo ya kidigitali au eneo lolote unaloona zitakuwa salama,” amesisitiza Nkwama.

Pia ameeleza kuwa Tume ya Utumishi wa Walimu ipo kwa ajili ya kuwahudumia walimu katika masuala ya Ajira, maadili na Maendeleo ya walimu, hivyo pale wanapohitaji huduma yoyote watumie njia mbalimbali za mawasiliano za Tume hiyo katika kuwasilisha hoja zao.

“Nisisitiza tena, walimu wetu msiwe na wasiwasi tume ipo kwa ajili ya kuwahudumia katika masuala ya ajira, maadili na maendeleo yenu, kwa hiyoo chochote utakachoona kinahitaji ufafanuzi milango iko wazi. Unaweza ukaingia kwenye tovuti yetu www.tsc.go.tz au kwenye barua pepe ya Katibu wa Tume, secretary@tsc.go.tz ukaweka jambo lako hapo nasi tutalipokea na kulifanyia kazi wa wakati. Au hata kwa kupiga simu, sisi tunafanya kazi muda wote,” amesema Katibu huyo.

Mwl. Nkwama alihitimisha kwa kusisitiza walimu kuzingatia miiko na maadili ya kazi na kufanya kazi kwa bidii, weledi, ubunifu na uzalendo kwa ajili ya kuinua kiwango cha taaluma kwa wanafunzi huku akisisitiza walimu kuwa na mwenendo mwema na mfano wa kuigwa katika jamii.

“Mwalimu ni mzazi na ni mlezi kwa wanafunzi, hivyo tunatarajia awe mfano kwa jamii. Tumepewa kazi kubwa ya kulea na kuelimisha watoto wa kitanzania, hivyo tuhakikishe tunatekeleza jukumu hilo kwa weledi huku tukimtanguliza Mwenyezi Mungu atusaidie tuweze kulitekeleza kwa kadiri ya mapenzi yake. Kizazi hiki cha wantanzania kiko mikononi mwetu sisi walimu,” amesisitiza.