WANAFUNZI 1,073,941 WACHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA MWAKA 2023

03 Jan, 2023
WANAFUNZI 1,073,941 WACHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA MWAKA 2023

Wanafunzi 1, 073, 941 waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022 wakiwemo wavulana 514, 846 na wasichana 559, 095 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2023.

 

Taarifa iliyotolewa Desemba 14, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Angellah Kairuki imesema kuwa idadi ya wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza Januari 2023 imeongezeka kwa wanafunzi 166, 139 sawa na ongezeko la asilimia 18.30 ikilinganishwa na wanafunzi 907, 802 walopata alama ya kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022.

 

Kati ya waliofaulu na kupangiwa kujiunga na kidato cha kwanza wamo wanafunzi wenye mahitaji maalum 2, 775 sawa na asilimia 0.26 ambao kati yao wavulana ni 1, 491 na wasichana 1, 284.

 

Waziri alisema kuwa Uchaguzi wa Wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Kwanza umefanyika kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Students Selection-Management Information System) ulioundwa na wataalam wa TEHAMA wa Ofisi ya Rais TAMISEMI na Baraza la Mitihani la Tanzania ambapo alisema mfumo huo umekuwa na faida mbalimbali.

 

“Mfumo huu umesaidia Kupunguza muda unaotumika kwenye Uchaguzi wa Wanafunzi; Kupunguza gharama zinazotumika wakati wa Zoezi la Uchaguzi na Upangaji wa Wanafunzi; na Kuongeza ufanisi na uwazi katika uchaguzi wa Wanafunzi kwa maana ya kuwa kila Mwanafunzi anapangwa kwenye Shule kulingana na Mwongozo wa Uchaguzi unavyoelekeza,” alisema.

 

Alifafanua kuwa Uchaguzi wa Wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka, 2023 umezingatia kigezo cha ufaulu wa mtahiniwa anayechaguliwa ambapo kila mtahiniwa aliyefanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mwaka, 2022 na kupata jumla ya alama za ufaulu kati ya 121 hadi 300 amechaguliwa na kupangiwa Shule ya Sekondari ya Serikali.

 

“Shule za Sekondari za Serikali walizopangiwa wanafunzi ziko katika makundi makuu mawili: Shule za Bweni na Shule za Kutwa. Kwa upande wa shule za bweni, shule hizi zimegawanywa katika makundi matatu ambayo ni Sekondari za Bweni za Wanafunzi wenye ufaulu wa Juu Zaidi (Special Schools), Shule za Sekondari za bweni - Ufundi na shule za Sekondari za Bweni Kawaida. Shule za Bweni ni za Kitaifa na hivyo, zimepangiwa kupokea Wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa kuzingatia mgawanyo wa nafasi uliobainishwa na vigezo vilivyowekwa ili kuimarisha Utaifa,” alifafanua.

 

Jumla ya Shule za Sekondari 4,309 zimepangiwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza, kati ya hizo Shule 38 sawa na asilimia 0.88 ni shule za bweni za kitaifa na Shule 4,271 sawa na asilimia 99.12 ni shule za kutwa.

 

Katika kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza, Darasa la Kwanza na Elimu ya Awali wanapata haki yao ya elimu ipasavyo, Waziri Kairuki alitoa maelekezo kwa viongozi wa ngazi ya Mikoa na Halmashauri.


Kwanza, alielekeza kuwa Wanafunzi wote waliochaguliwa wanaanza masomo yao tarehe 9 Januari, 2023, hivyo aliwaagiza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha maandalizi yote ikiwemo ujenzi wa miundombinu yote kwa ajili ya kuwapokea Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka, 2023 inakamilika kabla au ifikapo tarehe 24 Desemba 2022.


Pili, aliagiza kuwa Wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na shule za bweni waripoti shuleni ifikapo tarehe 07 Januari, 2023; na kwa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na shule za kutwa waripoti shuleni ifikapo tarehe 09 Januari, 2023 huku akiwaelekeza viongozi kuhakikisha Wazazi/Walezi na Jamii wanahimizwa kushirikiana na Uongozi wa Wilaya, Halmashauri na Shule ili wanafunzi wote waliochaguliwa wanaandikishwa, wanahudhuria na kubakia Shuleni hadi watakapohitimu Elimu ya Sekondari.

 

Tatu, aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, Viongozi na Watendaji wa Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa elimu kusimamia uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya Awali na Msingi na kuhakikisha uandikishwaji huo unakamilishwa ifikapo tarehe 31 Disemba 2022.